Kulikuwa na moto wa maneno kati ya Cristiano Ronaldo na kipa wa zamani wa Liverpool, Caoimhin Kelleher, kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Ureno na Ireland, uliochezwa jana usiku.
Ingawa Ronaldo alikosa penalti katika dakika ya 76 baada ya Kelleher kuokoa kwa ustadi kwa kutumia mguu, hatimaye Ureno waliondoka na ushindi wa 1-0 kupitia kichwa cha Ruben Neves aliyefunga dakika ya 91 bao lililowezesha timu hiyo kuendeleza rekodi ya ushindi wa mechi tatu mfululizo.
Kelele kati ya Ronaldo na Kelleher
Wakati mchezo ukiendelea, kamera zilinasa mvutano kati ya wawili hao. Ronaldo alionekana kukasirishwa na kipa huyo wa Brentford kwa kupoteza muda, jambo lililomfanya nyota huyo wa Al-Nassr kwenda kumwekea mpira na kumpigia makofi huku akimwambia aharakishe.
Kelleher, kwa utulivu wa hali ya juu, alimjibu Ronaldo kwa dharau kisha akaendelea kupoteza muda wake. Tukio hilo liliongeza joto la mchezo kabla ya kipa huyo kuokoa penalti ya Ronaldo dakika chache baadaye na kusherehekea kwa mbwembwe mbele ya mashabiki.
Hata hivyo, Ronaldo na Ureno walipata kisasi dakika za majeruhi kupitia Neves, ambaye alifunga kwa kichwa safi na kusherehekea kwa kuonyesha tattoo mpya aliyochora kumuenzi Diogo Jota, aliyefariki dunia miezi michache iliyopita.
Ireland yazidi kulemewa
Kocha wa Ireland, Heimir Hallgrímsson, alisema timu yake ilistahili angalau alama moja kutokana na jinsi walivyopambana.
“Tulicheza kwa kujituma sana, hasa kwenye ulinzi. Tulichoka mwishoni na Ureno wakapata nafasi ya kufanya pasi bora iliyotupa hasara. Tunapaswa kuwa na fahari, si furaha, kwa jinsi tulivyopambana,” amesema kocha huyo.
Ireland sasa imesalia nafasi ya mwisho kundi F, ikiwa na alama moja tu baada ya mechi tatu, huku Ureno wakiendelea kileleni wakiwa na alama tisa.
Ronaldo bado anatamani makombe
Licha ya kukosa penalti, Ronaldo (40) bado anaendelea kuwa hatari uwanjani. Nyota huyo amefikisha mabao 964 katika maisha yake ya soka, na anapania kufikisha 1000 kabla ya kustaafu.
Kwa kasi anayoendelea nayo katika klabu yake ya Al-Nassr na mkataba wake ulioongezwa hadi mwaka 2027, Ronaldo anaonekana kuwa na muda wa kutosha kufikia lengo lake hilo la kihistoria huku akipanga kutafuta taji la Kombe la Dunia mwakani Marekani, Canada na Mexico.