Fainali ya Ngao ya Jamii Wanawake inayozikutanisha Simba Queens na JKT Queens leo Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, imebeba mambo mawili. Kisasi na heshima.
Hiyo inatokana na mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye fainali ya Ngao ya Jamii mwaka 2023, Simba Queens iliibuka mbabe kwa penalti 5-4 dhidi ya JKT Queens baada ya dakika tisini matokeo kuwa 1-1.
Mechi hii inasubiriwa kwa hamu kubwa, lakini kabla ya fainali, itatanguliwa na mechi ya kusaka nafasi ya tatu kati ya Yanga Princess dhidi ya Mashujaa Queens.
Simba Queens na JKT Queens zimekuwa zikitawala soka la wanawake hapa nchini tangu Ligi Kuu Soka Wanawake ianzishwe mwaka 2017, na kila zinapokutana ni kama vita ya majirani wanaogombea mpaka wa ardhi. Hii ni mechi ya heshima, motisha na mwanzo mpya wa msimu inayotazamwa na wengi kama kipimo cha nani atakuwa bora msimu wa 2025-2026.
FAINALI YA KIBABE
Hii ni mara ya pili timu hizo zinakutana kwenye fainali ya michuano hiyo. Mara ya kwanza ilikuwa 2023 yalipozinduliwa mashindano hayo kwa mara ya kwanza na Simba Queens ikaibuka mabingwa.
Fainali hiyo ilipigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, Simba Queens ilinyakua taji hilo baada ya kuitandika JKT Queens kwa mikwaju ya penati 5-4 kufuatia sare ya 1-1.
Mara hii zinakutana tena. Simba Queens imetinga hatua hiyo baada ya kuichapa Mashujaa Queens mabao 2-0.
JKT Queens ilicheza mechi ya kusisimua dhidi ya Yanga Princess ambapo ilitoka sare ya 1-1, kabla ya kuibuka na ushindi kwa mikwaju ya penati 6-5.
Simba Queens ilionyesha ubora kwenye safu ya ushambuliaji na uimara wa safu ya ulinzi. Ushindi huo ulionyesha namna timu hiyo inavyoweza kumaliza mechi mapema tofauti na misimu miwili iliyopita.
Fainali inazikutanisha timu ambazo zina uzoefu na ushindani mkubwa kuanzia ligi ya ndani hadi michuano ya ukanda wa CECAFA, ziliposhiriki mara kadhaa na kufanya vizuri.
Fainali kati ya JKT Queens na Simba Queens inatarajiwa kuwa ya kibabe, ya kisasi na yenye ushindani wa hali ya juu si tu kwa sababu ni Ngao ya Jamii, bali kwa kuwa timu hizi ndizo zinazotawala soka la wanawake Tanzania kwa sasa.
Hii si mechi ya kawaida, ni fainali ya hadhi ambayo itaamua nani anaingia msimu mpya na heshima ya kuwa bingwa kwenye soka la wanawake.
Simba Queens na JKT Queens ndizo timu zilizomaliza juu kwenye ligi msimu uliopita, zote zikimaliza na pointi 47, lakini wanajeshi hao walikuwa na faida ya mabao ya kufunga, ikiweka kambani 70 na kuruhusu saba pekee, huku kinadada wa Msimbazi wakifunga 57 na kuruhusu 15.
Kila timu ina kikosi kilichojaa nyota wa kimataifa na wazawa wenye vipaji vikubwa. Hata hivyo, historia ya ushindani kati ya timu hizi ni ya muda mrefu tangu ligi ianze mwaka 2017 na zinapokutana, mechi huwa ngumu kutabirika.
Inatarajiwa kuwa mechi ya ushindani inayotumia akili zaidi kuliko nguvu. Si ajabu tukishuhudia mabao machache, lakini mpira wa kuvutia na inaweza kuamuliwa na makosa madogo, mipira ya kutengwa au hata penati.
MBINU ZA MAKOCHA
Hapa ndipo ilipo mechi yenyewe, mbinu za makocha wa timu hizo zitaamua nani anakwenda kunyakua taji hilo kwa mara nyingine.
Timu zote mbili zimeanza msimu zikiwa na makocha wapya. Kwa JKT Queens ikiwa chini ya Kessy Abdallah ambaye alichukua mikoba ya Ester Chabruma aliyeipa timu hiyo taji msimu uliopita, huku Simba Queens ikimpa mkataba Elieneza Nickolaus ambaye anaziba nafasi ya Mghana, Yussif Basigi.
Kocha wa Simba Queens ni mtaalamu wa kushambulia. Hupendelea mfumo wa 4-3-3 au 4-2-3-1, akiwatumia viungo wenye kasi kama Elizabeth Wambui na Aisha Mnunka na mawinga aina ya Zainah Nandede kupanua uwanja.
Simba Queens hucheza kwa ‘high pressing’ ikilazimisha makosa kwa wapinzani eneo lao la ulinzi. Mechi ya nusu fainali hakukuwa na maelewano eneo la umaliziaji lakini mawinga na viungo walifanya kazi kubwa ya kulazimisha kutengeneza nafasi.
Kocha Kessy ni msomi wa mchezo na hupendelea nidhamu ya kiuchezaji kuliko mbwembwe. JKT Queens hupanga timu kwa muundo wa kujilinda vizuri, kisha kushambulia kwa kasi. Anaamini katika mipira ya kushtukiza akitumia wachezaji wa katikati kama Winifrida Gerald, Donisia Minja kulazimisha wapinzani waingie kwenye mfumo wake kabla ya kushambulia kwa kasi.
Katika mechi kubwa kama hii, Kessy anaweza kubadili mfumo na kucheza kwa 4-5-1 ili kumiliki kiungo na kupunguza kasi ya Simba Queens, hasa upande wa kulia ambako anacheza mshambuliaji wa wapinzani wake Jentrix Shikangwa.
NYOTA WA KUCHUNGWA
Kwenye fainali hiyo kuna wachezaji wa kuangaliwa na kama watadhibitiwa vizuri huenda wasilete madhara kwa timu zote mbili. Kwa upande wa Simba Queens, Shikangwa ni miongoni mwao.
Mkenya huyo ni mshambuliaji hatari, ana spidi, ana chenga na mguu wa kulia unaoweza kufungua lango muda wowote. Ni mchezaji ambaye anaweza kuamua mechi kwa dakika. Mechi ya nusu fainali licha ya kuwa hajafunga bao dhidi ya Mashujaa, lakini alitoa asisti na kuleta changamoto kubwa kwenye eneo la ulinzi la timu hiyo.
Mara ya mwisho zilipokutana timu hizo kwenye ligi, JKT Queens ikiwa nyumbani ilipoteza mabao 4-3 na Shikangwa alifunga hat-trick, akamaliza msimu na mabao 24. Ndani ya misimu mitatu aliyocheza Ligi ya Tanzania, amekuwa akiingia kwenye orodha ya wafungaji bora wa WPL.
Mchezaji mwingine ni winga machachari, Winifrida Gerald wa JKT Queens, ambaye kila anapokuwa na mpira ni ngumu kwa mabeki wa timu pinzani kumpokonya. Ni mchezaji anayetumia akili, hivyo ukitumia nguvu unaweza kusababisha kumchezea faulo kutokana na kasi yake.
Ana uwezo wa kuusoma mchezo na kugawa mipira. Kwa sasa ndiye injini ya JKT Queens. Kupitia kwake, mpira huanzia na kumalizikia, hasa kwenye mashambulizi ya kushtukiza.
Umbo lake dogo limefanya mabeki wengi wa WPL kushindwa kumdhibiti ipasavyo. Amekuwa akipita kama upepo na kuwapita wapinzani na kupeleka mpira mbele haraka. Kasi na akili ndiyo silaha yake kubwa.
Wachezaji wengine ni mshambuliaji kinda Jamila Rajabu ambaye ndiye tegemeo eneo hilo. Uwezo wake wa kufunga kwa kichwa na miguu umekuwa tishio WPL tangu msimu uliopita, akimaliza na mabao 10. Pia kwenye mashindano ya CECAFA alimaliza kama mfungaji bora akiweka kambani mabao matano, hivyo ni mmoja ya wachezaji wa kuangaliwa.
Mwingine ni Elizabeth Wambui. Winga mwenye kasi, ana uwezo wa kupiga krosi na kuingia ndani ya boksi. Sio mzuri sana wa kufunga lakini anaweza kuvumbua njia mpya za kupenya ngome ya wapinzani. Anajua kutumia nafasi ndogo kutengeneza nafasi kubwa.
MECHI YA MAPEMA
Kabla ya fainali, mechi itakayopigwa mapema ni ya kusaka nafasi ya tatu kati ya Yanga Princess dhidi ya Mashujaa Queens, kuanzia saa 6 mchana.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa viungo wa Yanga Princess, Brenda Chaoor, alisema: “Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunamaliza nafasi ya tatu kwenye mashindano haya. Tumewaangalia wapinzani wetu na tumecheza nao kwenye mechi ya kirafiki, kwa hiyo tunawajua. Tutamkosa Wincate Kaari ambaye alipata kadi nyekundu mechi iliyopita.”
Nahodha wa Mashujaa Queens, Sabina Emmanuel alisema: “Tunaiheshimu Yanga, ni timu nzuri na sisi tunakwenda kutimiza yale tuliyoagizwa na kocha wetu. Tunaamini utakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa.”
Mussa Mgosi, ambaye ni kocha msaidizi wa Simba Queens, alisema: “Taswira ya ligi inaanza kwenye mechi za Ngao ya Jamii. Hivyo, msimu uliopita tulikosa mataji yote mawili kutokana na kutojiandaa vizuri. Kila mechi ina maandalizi yake na fainali siku zote huwa na ladha tofauti.”
Mchezaji wa JKT, Janeth Pangamwene, alisema: “Mechi na Simba huwa ngumu. Mechi iliyopita hatukucheza vizuri lakini tayari tumerekebisha mazoezini. Tunaamini tunacheza na timu bora kama Simba. Hivyo sisi kama mabingwa watetezi, kesho (leo) tuna kazi ya kutetea taji letu na kuwapa furaha mashabiki zetu.”