Yanga Princess imehitimisha michuano ya Ngao ya Jamii ya Wanawake kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa Queens, mchezo uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Wanawake, Yanga ilimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya JKT na Simba, huku Mashujaa ikimaliza nafasi ya nne.

Yanga chini ya kocha Edna Lema ‘Mourinho’ ilicheza mshindi wa tatu baada ya kutolewa hatua ya nusu fainali na JKT Queens kwa mikwaju ya penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1.

Katika mchezo huo, Edna alifanya mabadiliko kwenye maeneo matatu, eneo la golikipa akianza na Ester Emily aliyechukua nafasi ya Zubeda Mgunda aliyeanza mechi ya nusu fainali, kiungo akianza Adebis Ameerat aliyempisha Agnes Pallangyo aliyekuwa benchi.

Eneo lingine beki wa kushoto alianza Protasia Mbunda baada ya Wincate Kaari mechi iliyopita kuonyeshwa kadi nyekundu na upande wa kulia alicheza Diana Mnally akichukua nafasi ya Wema Maile ambaye hakuwepo kabisa kwenye benchi.

Timu hiyo ilionyesha kiwango bora tangu dakika za mwanzo, ikimiliki mpira na kushambulia kwa kasi kupitia viungo wake wa pembeni.

Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 16 kupitia kwa Jeanine Mukandayisenga aliyemalizia kwa utulivu krosi iliyochongwa na Precious Christopher baada ya ukuta wa Mashujaa Queens kujichanganya.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi huku Mashujaa Queens wakijaribu kurejea mchezoni, lakini juhudi zao ziligonga mwamba kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga Princess iliyoongozwa na nahodha Igwe Uzoamaka.

Dakika ya 48 Precious aliiongezea Yanga bao la pili akimalizia pasi ya Mukandayisenga, dakika 18 baadaye Aregash Kalsa akaweka kambani bao la tatu ndani ya boksi baada ya kumalizia pasi ya Adebis Ameerat. Hata hivyo kipindi cha kwanza cha mchezo huu, Yanga ilikosa mkwaju wa penalti.

Kwa ushindi huo, Yanga Princess imemaliza nafasi ya tatu katika Ngao ya Jamii ya Wanawake, michuano ambayo hufungua msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *