Dar es Salaam. Kitendo cha wimbo wa Marioo, Nairobi (2024) kuwa miongoni mwa zile zilizoingia katika mchakato wa kupata kazi chache zitakazowania tuzo za 68 za Grammy 2026, ni mafanikio makubwa kwa albumu yake pili.
Wimbo huo aliomshirikisha Bien, mwanachama wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya, umewasilishwa katika kipengele cha Best African Music Performance kinachobeba muziki wa Afrika pekee.
Novemba 7, ndipo majina ya wasanii watakaowania Grammy yatatangazwa, kisha tuzo hizo kutolewa Jumapili ya Februari 2, 2026 katika ukumbi wa Crypto.com Arena huko Los Angeles nchini Marekani.
Awamu hii wanamuziki kadhaa wa Bongofleva wamepita katika mchujo wa awali, baadhi yao ni AY, Fid Q, Diamond Platnumz, Abigail Chams na Harmonize ambaye amevusha nyimbo nne.
Wasanii wote hao wamejitosa katika kipengele kimoja na Marioo ambacho kwa mara ya mwisho mshindi wake alikuwa mkali wa Afrobeat kutokea Nigeria, Tems kupitia wimbo wake maarufu, Love Me Jeje (2024).
Marioo, mwanzilishi wa Bad Nation Records Label, ni mara ya kwanza wimbo wake kufika hatua hiyo katika tuzo za Grammy ingawa haijulikana iwapo hapo awali aliwahi kuwasilisha kazi zake ili kupata uteuzi.
Wimbo ‘Nairobi’ ambao ndio umempa heshima hiyo, ndio uliofanya vizuri zaidi katika katika albamu yake ya pili, The God Son (2024) ambayo mtoto wake, Princess Amarah ametajwa kama Mtayarishaji Mkuu.
Mathalani, katika mtandao wa YouTube imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 38 ndani ya miezi tisa, huku akipanda hadi nafasi ya pili katika orodha ya video za Marioo zilizofanya vizuri YouTube kwa muda wote.
Tangu wimbo huo uliotayarishwa na Kaniba Creator unatoka, ulipokelewa na wengi vizuri na ndio sababu Marioo aliutumbuiza katika hafla ya tuzo za Trace 2024 zilizofanyika Zanzibar kwa mara ya kwanza.
Nairobi ni wimbo unaoelezea maisha ya kijamii, mapenzi na mitindo ya maisha katika jiji la Nairobi, Kenya. Marioo anaelezea jinsi jiji hilo limejaa watu wenye mitazamo tofauti hasa kuhusu mapenzi, fedha na starehe.
Kwa kifupi ni wimbo wa kustarehesha na wenye ujumbe mwepesi unaochanganya mapenzi, maisha ya kisasa na ladha ya muziki wa Afrika Mashariki kama Bongofleva na Gengetone.
Mara ya kwanza ulisikika baada ya Marioo kuachia albamu yake ya pili, The God Son (2024) iliyotoka ikiwa na nyimbo 17, huku ikishirikisha mastaa kama Alikiba, Aslay, Bien, Kenny Sol, King Promise, Patoranking na kadhalika.
Ikiwa utafanikiwa kuchaguliwa kuwania Grammy 2026, basi Marioo atakuwa mwanamuziki wa kwanza wa Bongofleva kuwania tuzo hizo zenye hadhi ya juu zaidi duniani zikiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 65.
Hayo hayatakuwa mafanikio ya Marioo peke yake, bali tasnia nzima ila kubwa zaidi ni kwa albamu yake hiyo aliyotangazaja ujio wake pindi aliposhinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 zilizotolewa mwaka uliopita.
Marioo anaamini mradi huo utashinda tuzo ya TMA 2024 katika kipengele cha Albamu Bora, na ndio sababu alitumia jukwaa hilo kutangaza ujio wake, huku kwa upande mwingine akituma salamu sehemu fulani.
Hiyo ni baada ya albamu yake ya kwanza, The Kid You Know (2022) kushindwa kunyakua TMA 2022 kitu kilichopelekea kulalamika akidai amehujumiwa maana alistahili ushindi kwa asilimia kubwa.
Katika TMA 2022, ushindi wa Albamu Bora ulienda kwa Barnaba Love Sounds Different (2022), na ndipo Marioo akalalamika, kitu kilichopelekea Barnaba kumwambia akachukua tuzo hiyo kama anahisi alistahili.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba albamu hiyo Barnaba ambayo mtayarishaji mkuu ni Diamond, kwa jicho la kawaida tu ilistahili kushinda kutokana ilisheheni kazi nyingi ambazo zilikuja kufanya vizuri baadaye.
Pia ilishirikisha wasanii wengi wakubwa, miongoni mwao ni Jux, Alikiba, Diamond, Nandy, Rayvanny, Phina, Jay Melody, Kusah, Young Lunya, Mbosso, Khaligraph Jones, Joel Lwaga, Khadija Kopa, Lady Jaydee na kadhalika.
Hivyo lengo la Marioo tangu mwanzo lilikuwa ni kushinda tuzo ya TMA kupitia albamu hiyo, lakini hili la kufikia Grammy, ni wazi kuwa mradi huo umefanikiwa kupitia matarajio yake.
Ikumbukwe tangu Marioo ametoka na kibao chake, Dar Kugumu (2018), hajashinda tuzo yoyote kubwa ya kimataifa licha ya jitihada za kushirikiana na wasanii wa nje kutoka mataifa kama Afrika Kusini, Nigeria na kadhalika.