Hatua ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa Bara la Afrika imefika ukingoni, huku Cape Verde na Cameroon zikitarajiwa kupambana vikali leo kuwania nafasi ya mwisho ya kufuzu moja kwa moja kutoka Kundi D.

Cape Verde, maarufu kama Blue Sharks, ilishindwa kutumia nafasi ya kufuzu mapema baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Libya mjini Tripoli, jambo lililowafanya Simba Wasiofugika wa Cameroon kuendeleza matumaini yao kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mauritius.

Licha ya sare hiyo, Cape Verde bado ina nafasi nzuri zaidi ya kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yao ya soka. Iwapo itapata ushindi kwenye mechi ya leo ikiwa nyumbani dhidi ya Eswatini utatosha kuipeleka moja kwa moja kwenye michuano ya dunia itakayofanyika Marekani, Kanada na Mexico mwaka 2026.

Kwa upande mwingine, Cameroon ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18, nyuma ya vinara Cape Verde yenye pointi 20. Ili kufuzu, lazima washinde dhidi ya Angola jijini Yaoundé huku wakiiombea mabaya Cape Verde wapoteze au watoke sare, jambo ambalo ni gumu kutokea.

Cape Verde ilivyopoteza ushindi Tripoli

Mchezo dhidi ya Libya ulikuwa wa aina yake. Bao la kujifunga la Pico liliwapa wenyeji uongozi mapema kabla ya Telmo Arcanjo kusawazisha kwa kichwa.

Ezzeddin El Maremi aliwaweka Libya mbele tena kupitia mpira wa adhabu uliozama wavuni na kufanya matokeo kuwa 3-1.

Hata hivyo, Cape Verde walirudi mchezoni dakika za mwisho. Lopes Cabral alipunguza tofauti kufuatia makosa ya kipa, na Willy Semedo akasawazisha dakika ya 82 na kuipa timu yake alama moja muhimu ugenini.

Cameroon ilivyofufua matumaini

Katika uwanja wa Côte d’Or National Sports Complex, Saint-Pierre, Cameroon ilipata ushindi muhimu dhidi ya Mauritius. Nicolas Ngamaleu alifungua ukurasa wa mabao kipindi cha pili.

Bryan Mbeumo aliihakikishia Cameroon pointi tatu katika dakika za nyongeza baada ya kutupia wavuni bao la pili. Ushindi huo uliihakikishia timu hiyo kubaki kwenye kinyang’anyiro cha kufuzu hadi leo dakika 90 zitakapoamua.

Angola na Guinea-Bissau zatupwa nje

Katika michezo mingine ya kundi hilo, Angola ilibaki nje ya mbio za kufuzu baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Eswatini. Justice Figuareido aliifungia Eswatini mabao mawili kabla ya Jonathan Buatu na Ary Papel kuisawazishia Angola kwa mabao ya vichwa dakika za lala salama.

Wakati huo huo, Guinea-Bissau ilimaliza kampeni yao kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ethiopia, iliyopata ushindi wao wa kwanza kupitia bao la kichwa cha Ramkel Jemes Gang dakika ya 25.

Mchezo wa maamuzi

Cape Verde itakuwa mwenyeji wa Eswatini mjini Praia, huku Cameroon ikiikaribisha Angola jijini Yaoundé. Libya itamaliza ratiba kwa kucheza na Mauritius.

Kwa mujibu wa kanuni, ni vinara wa kundi pekee watakaofuzu moja kwa moja, hivyo Cape Verde wana nafasi ya kujihesabu miongoni mwa mataifa yatakayocheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza lakini lazima wapate ushindi dhidi ya Eswatini.

Cameroon kwa upande wao, wanasubiri miujiza kwani watapata nafasi ya kufuzu moja kwa moja iwapo watashinda dhidi ya Angola wakati Cape Verde watatoa sare au kupoteza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *