
Cape Verde limekuwa taifa la sita Afrika kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya leo, Oktoba 13, 2025 kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Eswatini.
Kabla ya Cape Verde, mataifa ya Tunisia, Misri, Ghana, Morocco na Algeria yalishanasa tiketi tano za kuiwakilisha Afrika katika fainali hizo zitakazofanyika Marekani, Mexico na Canada mwakani.
Taifa hilo ambalo ni kisiwa kilichopo Magharibi mwa Afrika kililazimika kusubiri hadi katika dakika 45 za kipindi cha pili, kupata mabao hayo matatu ambayo yamewahakikishia uongozi wa kundi D wakifikisha pointi 23 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi hilo.
Mabao ya ushindi ya Cape Verde katika mchezo wa leo yamefungwa na nyota wa Verona anayecheza kwa mkopo katika timu ya Casa Pia, Rocha Livramento, lingine limepachikwa na mshambuliaji wa Omonia ya Cyprus, Willy Semedo na bao la tatu kimefungwa na Stopira.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya taifa ya Cape Verde kufuzu Fainali za Kombe la Dunia na itakuwa timu ya 14 barani Afrika kuwahi kushiriki Fainali hizo.
Mataifa mengine 13 ya Afrika ambayo yamewahi kushiriki Kombe la Dunia ni Ghana, Morocco, Angola, Togo, Afrika Kusini, Algeria, Tunisia, DR Congo, Senegal, Nigeria, Cameroon, Misri na Ivory Coast.
Mchezo huo wa leo ambao Cape Verde wameutumia kuandika historia, ulichezeshwa na marefa kutoka Tanzania wakiongozwa na refa wa kati, Ahmed Arajiga.
Mohamed Mkono alikuwa ni refa msaidizi namba moja huku namba mbili akiwa ni Hamdani Said na Nasir Siyah akiwa refa wa akiba.
Arajiga amemaliza mchezo huo akiwa ametoa kadi tano za njano ambapo mbili amewaonyesha wachezaji wa Cape Verde na tatu amewaonyesha wachezaji wa Eswatini.