Kiungo mshambuliaji wa Barcelona, Ferran Torres amelazimika kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa ya Hispania, baada ya kubainika hataweza kucheza mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bulgaria.
Hispania inayoongoza Kundi E, itakuwa mwenyeji wa mechi hiyo, itakayopigwa kesho Jumanne, Oktoba 14, 2025 kwenye Uwanja wa José Zorrilla, mjini Valladolid.
Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Hispania (RFEF) imethibitisha kuwa kiungo huyo anasumbuliwa na maumivu ya misuli, na tayari ameshaondoka kambini kwa ajili ya matibabu yatakayosimamiwa na klabu yake ya Barcelona.

Inadaiwa kuwa, Torres alipata maumivu hayo kwenye mechi ya Hispania dhidi ya Georgia iliyopigwa juzi Jumamosi, Oktoba 11, 2025 ambapo La Roja iliibuka na ushindi wa 2-0, na kufikisha pointi 16 zinazoiweka kileleni.
“Ferran Torres ameondolewa kwenye kikosi kitakachocheza mechi ya nne ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 itakayofanyika Valladolid dhidi ya Bulgaria.
“Mshambuliaji wa FC Barcelona, baada ya kumaliza mechi dhidi ya Georgia huko Elche, aliripoti kuwa na maumivu ya misuli, ambayo yalitathminiwa na timu ya kitabibu ya RFEF, pamoja na kufanyiwa vipimo vya ziada, ambapo waligundua kuwa ni uchovu wa misuli bila jeraha lolote la kimaumbile.
“Kutokana na ukaribu wa mechi dhidi ya Bulgaria, na kwa kuzingatia sera ya kuepuka hatari na kuweka afya ya mchezaji hatarini, Torres ameondolewa kwenye kikosi. Timu ya matatibu ya kitabibu ya FC Barcelona imejulishwa suala hili,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo huenda ikawa shubiri kwa Barcelona, hasa ikizingatiwa kwa sasa kuna idadi kubwa ya wachezaji majeruhi, huku timu hiyo ikielekea kwenye mechi ya El Clasico itakayopigwa Oktoba 26, 2025.
Barcelona tayari imeshampoteza Dani Olmo kutoka kwenye kikosi cha Hispania wiki iliyopita kutokana na jeraha la nyama za paja, huku Lamine Yamal naye akijiondoa kwenye timu ya taifa kabla ya hapo.
Bado haijajulikana kama tatizo la Ferran ni kubwa kiasi gani na iwapo litaathiri upatikanaji wake kwa ajili ya mechi dhidi ya Girona mwishoni mwa wiki hii.