Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdul Kambaya amewatahadharisha Watanzania juu ya wanasiasa wa upinzani wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema siasa ni mashindano ya hoja, siyo matusi wala fujo.

Kambaya ametoa kauli hiyo leo  Oktoba 13, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Makurumla, Manispaa ya Ubungo ambapo aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaopotosha jamii kupitia mitandao.

“Siasa sio kushindanisha ukubwa wa sauti, hapana. Siasa ni kushindana kwa hoja. Kama wenzetu wana hoja, basi wazilete mezani, siyo kukaa mitandaoni na kuhamasisha watu kufanya maandamano wakati wao wenyewe hawaonekani,” amesema Kambaya huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Kambaya ameongeza kuwa baadhi ya watu wanaomchukia Rais Samia Suluhu Hassan, hawafanyi hivyo kwa sababu ya mavazi yake au jinsia yake, bali kutokana na uimara wake katika kushughulikia changamoto za wananchi na kasi ya maendeleo ambayo wengi hawakuitarajia.

“Wanaomchukia Samia wanachukia mafanikio yake. Wamezoea kuona wanawake wakinyamaza, lakini huyu mama ni jasiri, anajituma, anatatua matatizo ya wananchi kwa vitendo,” amesema.

Kambaya amewataka wananchi wa Makurumla kutoingia kwenye mtego wa watu wanaohubiri mambo yasiyotekelezeka, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika kata hiyo ni matokeo ya uongozi makini wa CCM na Rais Samia.

“Makurumla ya leo sio ile ya mwaka 2020. Samia na Serikali yake wamefanya kazi kubwa. Tazameni huduma za afya, maji, na elimu mabadiliko ni makubwa. Hata watoto wa shule leo wangeruhusiwa kupiga kura, wangemchagua Samia kwa sababu wanajua amani yao inayowafanya wasome itaendelea,” ameongeza Kambaya.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amewaomba wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Samia, akisema ndiye kiongozi mwenye uzoefu na uwezo wa kusimamia amani, umoja na maendeleo ya taifa.

“Samia ni kiongozi mwenye maono. Anatoka katika chama imara chenye historia ya kujenga nchi. Tumuunge mkono kwa kura zetu ili aendelee kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi,” amesema Profesa Kitila.

Amewaomba wananchi kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kusimamia miradi ya maendeleo na kupunguza kero za michango shuleni.

“Serikali ya Samia ilifuta ada zote, lakini bado kuna wazazi wanalalamika kuchangishwa ovyo. Nikichaguliwa tena, nitahakikisha tatizo hilo linaisha kabisa,” ameahidi Profesa Kitila.

Mgombea udiwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga amesema akichaguliwa ataendelea kushirikiana na mbunge na Serikali katika kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo miundombinu ya maji na ujenzi wa kingo za Mto China.

“Tutahakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati na kingo za Mto China zinajengwa ili kuzuia mafuriko. Tayari tumeona mafanikio kwenye mradi wa jengo la kujifungulia kina mama katika zahanati ya kata hii. Huo ndio mwelekeo wa CCM vitendo, si maneno,” amesema Kimwanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *