Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeitaja nchi ya Morocco kuwa mwenyeji wa mashindano ya mchujo ya Afrika yatakayozihusisha timu nne kwa ajili ya kuwania nafasi ya ziada kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Vinara wa makundi tisa ya kufuzu barani Afrika watatinga moja kwa moja kwenye fainali hizo zitakazofanyika Juni 2026. Hata hivyo, kuna njia nyingine ya kupata nafasi ya ziada kwa moja kati ya timu nne bora zilizoshika nafasi ya pili katika makundi yao.
Timu hizo nne zitashiriki mashindano mafupi, yatakayofanyika Morocco mwezi Novemba 2025, ambapo mshindi mmoja atapata nafasi ya kucheza mechi ya mchujo wa kimataifa (inter-continental playoff) mwezi Machi 2026 dhidi ya timu kutoka bara lingine kwa ajili ya kupata tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia la zitakazoshirikisha mataifa 48 kwa mara ya kwanza.
Ratiba na upangaji wa mechi
Majina ya timu nne zitakazoshiriki mashindano hayo ya awali ya Afrika yatathibitishwa baada ya ratiba ya makundi kukamilika kesho Jumanne.

Mechi za nusu fainali zitapigwa Novemba 13, 2025 kwenye viwanja ambavyo bado havijatajwa rasmi, na fainali itafanyika Novemba 16, 2025.
Upangaji wa mechi utafanyika kulingana na viwango vya ubora vya FIFA vitakavyotolewa Oktoba 23, 2025 ambapo timu iliyo juu zaidi itacheza na iliyo chini zaidi, na ya pili kwa ubora itachuana na ya tatu.
Hadi sasa Afrika imeshapata wawakilishi watano kwenye fainali za Kombe le Dunia 2026 ambao ni Morocco, Tunisia, Misri, Algeria na Ghana.
Leo Jumatatu, Cape Verde inaweza kufuzu iwapo itashinda dhidi ya Eswatini, huku Ivory Coast na Senegal pia zikiwa na nafasi ya kufuzu kesho Jumanne endapo zitaibuka na ushindi.
Katika Kundi C, mambo bado hayajawa wazi, ambapo Benin, Nigeria, na Afrika Kusini zote zina nafasi ya kufuzu zitakapocheza mechi zao za mwisho kesho Jumanne.