Liverpool, England. Staa wa zamani wa Ligi Kuu England, Michael Owen anaamini masupastaa Mohamed Salah na Alexander Isak watatiki na kufanya vizuri Liverpool, licha ya chama lao Liverpool kucheza chini ya kiwango.
Kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Chelsea kiliifanya Liverpool kushuka hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England tangu Septemba 2024.
Bao la dakika za majeruhi la Estevao lilitosha kuifanya Liverpool kukumbana na kipigo cha tatu mfululizo, ikiwa ni mwendelezo wa kufungwa mabao kwenye dakika za mwisho baada ya lile la Eddie Nketiah wa Crystal Palace.

Liverpool ya kocha Arne Slot ilikumbana na kipigo cha 1-0 kutoka kwa Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Arsenal, mchezo ujao, Liverpool inakabiliwa na mahasimu wao, Manchester United kwenye Ligi Kuu England wikiendi hii.
Kuna maswali mengi kuhusu kiwango cha Liverpool baada ya usajili mkubwa uliofanyika kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Liverpool ilivunja rekodi ya uhamisho kwenye Ligi Kuu England, wakati ilipomsajili Isak kwa Pauni 130 milioni, huku pia iliwanasa Florian Wirtz (Pauni 116milioni), Hugo Ekitike (Pauni 79milioni), Milos Kerkez (Pauni 40milioni), Jeremie Frimpong (Pauni 29.5milioni) na Giovanni Leoni (Pauni 26milioni).
Swali jingine ni kama usajili mpya wa mastraika unakwenda vizuri kucheza na supastaa wao, Salah, ambaye alionyesha kiwango kikubwa sana msimu uliopita.

Lakini, Owen, aliyewahi kuichezea Liverpool hana wasiwasi juu ya mastaa hao, akiwamo Isak na Mo Salah kwamba watacheza vizuri na kurudi kwenye viwango vyao bora.
Owen amesema: “Kuhusu washambuliaji wao, watakwenda kuwa vizuri. Mo Salah bila shaka atarudi kwenye kiwango chake, huwezi kumpuuza. Bado yupo fiti na hasumbuliwi na majeruhi.
“Cody Gakpo naye anacheza vizuri. Bila shaka Hugo Ekitike pia. Alexander Isak itarudi kwenye viwango vyake kwa sababu kwa sasa anasumbuka kwa kuwa hakuwa na pre-season nzuri.”