Dar es Salaam. Sekta ya afya nchini inaendelea kushuhudia mageuzi makubwa kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Septemba 15, 2025, jijini Dar es Salaam, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeandika historia mpya kwa kuzindua mfumo wa kidijitali wa kuweka miadi na madaktari.
Mfumo huo, unaojulikana kama “MOI Online Appointment System,” unalenga kuondoa usumbufu wa msongamano wa wagonjwa, huku ukileta urahisi wa kupata huduma kwa wakati.
Katika hafla ya uzinduzi wa mfumo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk Mpoki Ulisubisya, alieleza kwa kina sababu za kuanzishwa kwa mfumo huo. Alisema kwa miaka mingi, wagonjwa wamekuwa wakilazimika kufika hospitalini mapema asubuhi ili kujiandikisha kwa ajili ya kuonana na daktari.
Mara nyingine, wagonjwa wamejikuta wakipoteza muda na gharama, kwa sababu ya aidha kliniki husika haipo siku hiyo au daktari aliyekusudiwa hayupo. Hali hiyo ilisababisha malalamiko na kuathiri ustawi wa wagonjwa, hususan wanaosafiri kutoka mikoa ya mbali.
“Kwa sasa mgonjwa anaweza kumchagua daktari anayemtaka, siku na muda wa kumuona, na kliniki anayohitaji kupitia kwenye simu au kompyuta yake. Hii itapunguza kabisa adha ya wagonjwa kwenda hospitalini mara kwa mara bila ya mafanikio,” alisema Dk Mpoki kwa msisitizo.
Mfumo huu mpya unapatikana saa 24 kwa siku zote za wiki. Kupitia simu janja, laptop au kishikwambi, mgonjwa anatakiwa tu kuingia kwenye tovuti ya MOI (www.moi.ac.tz) au kiunganishi cha moja kwa moja miadi.moi.ac.tz/appointment, na kisha kuanza kujaza taarifa zake.

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Taasisi ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk Marina Njelekela.
Baada ya kujaza taarifa fupi kama jina na namba ya simu, mgonjwa anaweza kuendelea kuchagua huduma anayohitaji, daktari anayemtaka na muda unaomfaa. Mara baada ya kumaliza zoezi hilo, mgonjwa atapokea ujumbe mfupi wa maandishi, kuthibitisha miadi yake.
Lakini mfumo huu hauishii hapo. Endapo kutatokea mabadiliko kama vile daktari kupata dharura, mgonjwa atapokea taarifa kwenye simu yake mara moja.
Anaweza pia kuchagua daktari mwingine au kupanga siku nyingine bila kulazimika kufika hospitalini. Hili ndilo jambo linalofanya mfumo huu uwe wa kipekee, kwa kuwa unajali muda na kuheshimu mgonjwa.
Faida za mfumo
Mfumo huu mpya wa MOI unasaidia kuokoa muda unaopotezwa na wagonjwa hospitalini hapo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ambapo wagonjwa walilazimika kupanga foleni ndefu ili kuwahi huduma mapema.
Pili, mfumo huu unatoa uhuru wa kuchagua daktari anayemfaa mgonjwa, jambo ambalo awali lilikuwa gumu kwa sababu ya utaratibu uliopo wa hospitali hiyo. Tatu, wagonjwa wana uhakika wa kupata huduma kwa wakati kwa sababu miadi inathibitishwa moja kwa moja na mfumo huo.
“Mgonjwa baada ya kufanya miadi atapokea ujumbe mfupi wa simu ukimtaarifu kukubalika kwa miadi yake, na hata pale daktari husika atakapopata udhuru mteja atapata taarifa kwenye simu yake na kumwezesha kuchagua daktari mwingine au amsubirie kwa siku nyingine,” alifafanua Dk Ulisubisya.
Na la mwisho, mfumo unasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa wanaotoka mikoani kwani sasa wanaweza kupanga safari zao kwa uhakika wakijua miadi yao imekubaliwa. Kwa upande wa MOI, faida zake ni pamoja na kuimarisha upangaji wa ratiba za madaktari na kupunguza msongamano katika mapokezi.

Pia, taarifa za wagonjwa zitawekwa kwenye mfumo kwa mpangilio bora, hivyo kurahisisha ufuatiliaji na utoaji wa huduma. Kwa maneno mengine, mfumo huo siyo tu msaada kwa wagonjwa bali pia ni nyenzo ya kuongeza ufanisi ndani ya taasisi.
“MOI Online Appointment System” ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Serikali kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia matumizi ya teknolojia.
Mifumo kama hii inaonyesha kwamba Tanzania ipo kwenye njia sahihi ya kufikia malengo ya kidijitali, ambapo huduma zinapatikana kwa urahisi, uwazi na ufanisi zaidi. Ni hatua kubwa kuelekea kupunguza changamoto zilizokuwa zinawaumiza wagonjwa na kuathiri ufanisi wa taasisi kubwa kama MOI.
Hata hivyo, ili mfumo huu uwe na ufanisi wa kweli, elimu kwa wananchi inahitajika. Si kila mtu anafahamu jinsi ya kutumia simu janja au tovuti, hasa vijijini.
Hivyo, MOI kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya na teknolojia, inapaswa kuendelea kutoa hamasa na mafunzo kwa wananchi ili kuhakikisha mfumo huu unawafikia Watanzania wengi zaidi.