Akiwa kama Mwenyekiti wa Bodi, Crescentius Magori, ameiongoza klabu ya Simba kufanya moja ya maamuzi ya kubahatisha katika historia ya mpira wa Tanzania.

Kitendo cha klabu hiyo kumchukua kocha wa Gaborone United ya Botswana, Dimitar Pandev, raia wa Bulgaria na kumfanya kuwa kocha mkuu ni kuishusha thamani yao badala ya kuipandisha.

Hii ni kwa sababu kocha huyo hana vigezo vya kufundisha soka hapa nchini kutokana na kukosa elimu inayostahili.

Elimu yake ya ukocha ni Diploma A ya UEFA ambayo haikidhi kuwa kocha mkuu Tanzania na hata kufundisha kwenye mashindano ya Afrika.

Elimu inayotakiwa Tanzania na Afrika kuwa kocha mkuu ni Diploma A ya CAF au Pro License yoyote.

Cheti cha Pandev cha Diploma A ya UEFA kinahesabika sawa na Diploma B hapa Afrika na kinatosha kuwa kocha msaidizi tu.

Na hii ndio sababu Simba wamemtangaza kocha huyo kama meneja mkuu, ili kuikwepa sheria hii.

Wanataka ahesabike kama meneja ili asizuiliwe kukaa kwenye benchi wakati wa mechi na hiki ndicho Gaborone United walikifanya wakati wakicheza na Simba.

Sheria za CAF hazikumruhusu Pandev kukaa benchi la ufundi dhidi ya Simba kama kocha mkuu hivyo alikaa kama meneja wa timu.

Hili ni kosa kubwa sana ambalo Magori kama mwenyekiti wa Bodi, amelifanya. Amekubali kuruhusu klabu kufanya maamuzi ya kubahatisha ambayo yanaweza kuirudisha nyuma sana au kuitia hasara kubwa.

Naam, mpira ni mchezo wa kubahatisha (take risk) lakini sio kwa kiwango hiki walichofikia Simba.

Unaweza kufanya hivyo kwa kocha mwenye vyeti lakini hana uzoefu kama walivyofanya kwa Fadlu Davids, au mwenye uzoefu lakini hana vyeti!

Ila kwa Pandev hana vyote, hana vyeti na wala hana uzoefu wa kuishawishi klabu kubwa kama Simba kufumba macho kiasi hicho.

Magori ni kiongozi mzoefu wa mpira na matarajio yalikuwa kutumia uzoefu huo kwenye uongozi wake ili kuipeleka mbele klabu hiyo ambayo inateseka kwa kukosa ubingwa na kufungwa mfululizo na watani wao Yanga.

Wakati Yanga wakifikiria kumfukuza kocha wao, Romania Folz, asiye na uzoefu na kumchukua kocha wa Madagascar, Romuald Rakotondrabe, kutokana na mafanikio yake kwenye CHAN 2024, Simba wanamleta kocha asiye na vyeti.

Halafu wakifungwa kwa mara ya saba na Yanga waanze kulia na MANGUNGU. Sawa, Mangungu ni mwenyekiti wa klabu anayewakilisha wanachama, lakini mara zote anayemlipa mpiga zumari ndio huchagua wimbo.

Magori ndiye anayemlipa mpiga zumari kwa sababu anatoka upande wa mwekezaji, anayetoa pesa sauti kubwa itatoka kwake! Unaweza ukajiuliza, Simba wamekwama kupata kocha anayestahili?

Klabu kama Simba inatamaniwa na makocha wengi wenye sifa na uwezo, unaothibitishwa na rekodi zao na vyeti vyao. Lakini Magori akaiongoza bodi kumchukua kocha asiye na vyeti kwa sababu aliwasumbua.

Sasa wanachofanya ni kumsajili Seleman Matola kama kocha mkuu naam, ni jambo jema kwa wazawa lakini hiyo inatakiwa iwe katika uhalisia, sio kiujanja ujanja kama hivi.

Matola anapaswa kuwa kocha mkuu halisi, sio cheti chake kutumika kama mwamvuli wa kumfunikia Pandev.

Magori kaanza na mguu mbaya kwenye uongozi wake, uamuzi wake mkubwa wa kwanza ni SHOT OFF TARGET, tusubiri mengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *