
Dar es Salaam. Kuna kitu nimekiwaza washkaji. Inawezakana tunakichulia poa, lakini kinatuma ujumbe mmoja wenye nguvu sana kwa jamii. Jibu swali hili… taja wasanii wa muziki wa kike wakubwa zaidi Tanzania.
Hata kama umetaja majina ya wasanii 50 nina uhakika kuna majina ya wasanii wawili umetangulia kuyataja. Na ukweli ni kwamba hao ndiyo wasanii wa muziki wa kike wakubwa. Hao ndiyo wanatengeneza hits. Hao ndiyo wanaingia kwenye listi ambazo zina wanaume tu.
Listi kama wasanii wanaolipwa pesa nyingi. Wasanii waliosikilizwa sana kwenye ‘streaming platforms’ na kadhalika. Na ukitaka kuamini ni wakubwa naweza kuwazungumzia bila kuwataja majina, lakini bado ukawatambua.
Sasa naomba tutazame hadithi zao za mapenzi. Tuanze na aliyetangulia kuingia kwenye gemu. Yeye alianzia muziki kama zao la taasisi moja ya kuitwa Jumba la Vipaji Tanzania. Kiingereza tungeita Tanzania House of Talents.
Akaachia ngoma za hapa na pale ambazo kimsingi zilikuwa zinafanana na ngoma za wasanii wengi kutoka jumba hilo la vipaji. Lakini, ghafla akaanza kupata sapoti kubwa kwenye redio iliyokuwa inashirikiana na taasisi hiyo ya kulea na kukuza vipaji.
Kusapotiwa kwake kwa nguvu kukazua tetesi kwamba msanii huyo wa kike anatoka kimapenzi na mmoja wa mabosi wa redio hiyo na mlezi wa karibu kabisa wa Jumba la Vipaji Tanzania. Na tetesi zikathibitika miezi mingi baadaye pale ambapo mtu aliyekuwa anatajwa kutoka na msanii huyo alipomchumbia.
Kwa sasa wawili hawa hawapo pamoja kwa sababu mwanaume alishafariki dunia. Mungu amrehemu. Lakini, mwanamke amemuvu oni na sasa ameolewa na msanii mwenzake.
Kipindi tetesi za mahusiano na uchumba wao, msanii huyo alivuma na kuwa msanii wa kike mkubwa zaidi Tanzania. Ukweli ni kwamba hakuvuma kwa sababu ya kubebwa, hapana. Kipaji cha kuimba anacho tena kikubwa mno, lakini naomba tupige pozi hapo. Tutarudi baadaye kumalizia. Kwa sasa twende kwa msanii wa pili ambaye pengine ni mkubwa zaidi hivi tunavyozungumza.
Huyu yeye ni mtoto wa mwanamuziki maarufu na mkongwe Tanzania. Alichukuliwa na mama’ke na kupelekwa kwenye lebo kubwa zaidi ya muziki Tanzania na baada ya miaka mingi akiwa msanii wa nyuma ya pazia wa lebo hiyo akatambulishwa rasmi.
Baada ya miezi mingi ya kuvuma na kushikilia taji la msanii wa kike mkubwa zaidi Tanzania zikaanza kuvuma tetesi kwamba anatoka na bosi wake. Bosi wa lebo anayofanyia kazi. Tetesi zikaenda kama tetesi na kiki mpaka hivi majuzi wawili hao walipothibitisha kufunga ndoa na hivi ninavyokwambia wanaitana mke na mume.
Maisha ya mapenzi ya wawili hao yanatoa meseji kubwa ambayo ama tunaijua, ila tunajifanya hatuijui au tunaijua, lakini hatuna cha kufanya. Maisha ya mapenzi ya wawili hao yanazalisha maswali ya kwanini wasanii wakubwa wa kike Tanzania wana stori moja ya mapenzi ya kutembea na watu wanaowaunga mkono? Je hilo ni takwa kwa wasanii kike? Kwamba ili msanii wa kike awe mkubwa ni lazima atembee na bosi wake? Maana hatujawahi kusikia tetesi za Alikiba kutembea na bosi wake. Diamond kutembea na bosi wake. Marioo kutembea na bosi wake. Zaidi mabosi zao wa kike wanaishia kwenye kuwaita dada.
Na wala sisemi kwamba kuna rushwa ya ngono, hapana. Hawa ni watu wazima wawili wanaokubaliana na mwisho wao unaishia kuwa ndoa. Na pia sisemi kwamba hakuna rushwa ya ngono. Sijui kwanini wale wa kike wanakubali kuwa na mahusiano na mabosi zao.
Kama wanakubali kwa sababu za nje ya mapenzi hapo kuna harufu ya rushwa ya ngono. Lakini, mimi siongelei hilo kwa leo. Ninachosema ni kwamba kuna ujumbe wa kuubeba hapa au kama hatuwezi kubeba ujumbe, basi hata tubebe maswali pengine siku tukipata majibu ya maswali hayo tutakuwa tumepata na ujumbe wake.