Dar es Salaam. Hanstone ni msanii wa Bongo Fleva ambaye alipata umaarufu mkubwa kupitia wimbo maarufu wa ‘Lokote’ ambao alishirikishwa na Maua Sama. Wimbo huu ulipotoka mwaka 2018, uligeuka kuwa wimbo wa taifa kwa vijana, ukitamba kwenye redio, mitandao ya kijamii na hata kwenye klabu za burudani.
Licha ya kushirikishwa na Maua Sama ambaye ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri Bongo, sauti ya Hanstone kwenye wimbo huo iliwashtua wengi kwa ubunifu, uchezaji wa maneno na uimbaji wa kuvutia.
Msanii huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanamuziki marehemu Banza Stone, aliandika wimbo wote kuanzia kipande cha Maua Sama hadi verse yake ya pili.
‘Lokote’ haikuwa tu wimbo wa kawaida, ilikuwa ni ngoma ya kizazi. Ilizindua jina la Hanstone kwa haraka, ikampa nafasi ya kutambulika kama msanii anayeweza kufanikisha hit song hata akiwa bado chipukizi.
Ule mdundo wa Afro-pop na mahadhi yaliyokuwa pendwa kwa baadhi ya masikio ya wapenda burudani vilichangia kuufanya wimbo huo kuwa wa mafanikio ya haraka.
Pamoja na hayo, jamii ilimchukulia Hanstone kama msanii mpya chipukizi, mwenye uwezo wa kuteka soko la vijana. Alianza kuvutia vyombo vya habari kufanya naye mahojiano, shoo na ushirikiano wa kimuziki.
Baada ya wimbo huo kutamba, matarajio kwa Hanstone yalipanda makubwa. Watu walitegemea atoe vibao vingine vya kiwango sawa au zaidi ya Iokote. Hata hivyo, licha ya kutoa nyimbo kama Nimechoka, Yataniua, Acha Lipite na Washamba, hakuna hata mmoja ulioweza kufikia mafanikio ya Lokote.
Ni kama umaarufu wa ngoma hiyo ulikuwa ni maji ya shingo kwake mwenyewe, kwani hakuweza kutoa ngoma ya levo hizo tena wala muendelezo baada ya Lokote na matarajio ya wengi yalionekana kukwamia pale.
Sio kwamba hatoi ngoma, hapana zipo. Ni siku tano tu zilizopita tangu aachie kibao kipya cha Like akimshirikisha Rilvin lakini baadhi ya mashabiki hawajui na wengine labda washasahau kama msanii huyo yupo na anaendelea na kazi zake.
Menejimenti
Kutokuwapo na lebo au menejimenti imara ni moja ya sababu zilizomfanya Hanstone kukosa timu madhubuti ya kumsukuma kisoko au kumsaidia kujenga chapa binafsi.
Umaarufu wake ulijengwa kupitia kolabo. Hakuwa na msingi imara wa mashabiki waliomfuata kwa kazi zake binafsi na hiyo ni kutokana na ukosefu wa mikakati ya kujijenga mwenyewe nje ya wimbo huo.
Soko la Bongo Fleva linabadilika kila siku. Mfano kwa sasa muziki unaopendwa zaidi ni Amapiano ule wa asili ya Afrika Kusini. Hivyo, wasanii kama Marioo, Zuchu, Nandy na wengineo wanaendana na soko hilo ili waweze kupata mashabiki wengine na kubadilika.
Hanstone ameendelea kuimba aina ile ile ya muziki ambao baadhi ya mashabiki wamezoea kuisikia sauti yake na hata kwenye namba za watazamaji YouTube ziko chini tofauti na Lokote ambayo hadi sasa imeingiza watazamaji milioni 32.
Ishu ya Wasafi
Kuna kipindi zilizuka tetesi kwamba Hanstone yuko njiani kujiunga na Wasafi, lebo inayomilikiwa na nyota wa kimataifa Diamond Platnumz. Taarifa hizo ziliwafanya wengi kumwona kama msanii atakayefanya vizuri na kupata mafanikio makubwa kwenye muziki wake.
Lakini ndoto hizo hazikutimia. Sababu hazikuwa wazi kwa Wasafi, lakini baadhi ya maoni yalisema hakufikia vigezo vya kibiashara vya lebo hiyo, huku wengine wakidai hakuwa tayari kimikataba.
Baadaye Hanstone alionekana akitoa lawama kwa baadhi ya watu waliompa matumaini makubwa lakini wakamuacha bila msaada. Hii inaashiria pia kukata tamaa au kukosa muongozo sahihi, jambo ambalo limewahi kuwakumba wasanii wengi.
Kwenye moja ya mahojiano alisema “Nilikuwa narekodi wimbo na nilisainiwa Wasafi. Nilikuwa siingizi chochote zaidi ya kurekodi tu na nilikuwa na mkataba, hivyo kuna vitu nilikuwa sivifanyi hasa yanapotokea madili ya kazi. Nilikuwa nikikaa pale nikiomba pesa, sikuwa naingiza pesa, nikaamua kuondoka.”
Hanstone ni hadithi ya msanii aliyeonja umaarufu mkubwa kwa haraka, lakini akashindwa kushikilia pale pale ama kuopaa zaidi kwa haraka japo muda bado anao wa kufanya makubwa zaidi ya aliyoyafanya wakati akijitambulisha.
Hii ni changamoto ambayo imewakuta wasanii wengi wa kizazi hiki. Wapo wasanii kama Lody Music ambaye alitamba na wimbo wa Kubali, Wini, Lony Bway na wengine wengi ambao hawasikiki kwa ukubwa kama hapo awali.
Umaarufu wa ghafla bila msingi imara wa kibiashara, ubunifu endelevu au menejimenti madhubuti ni kati ya mitihani wanayokutana nayo wasanii wengi wachanga.
Swali ni je, Hanstone anaweza kurudi tena? Jibu ni ndiyo anaweza, kama atawekeza kwenye kujifunza zaidi tasnia na kuweka ubunifu mpya.