Wazazi wa mastaa wa soka Jude na Jobe Bellingham wametengana rasmi baada ya miongo miwili ya ndoa. Habari zilizoripotiwa na Daily Mail zinaeleza kuwa baba yao, Mark Bellingham, ambaye ni afisa wa zamani wa polisi, sasa yuko karibu na askari mwenzake wa zamani anayeitwa Shelley Punshon, mama wa watoto wawili kutoka Stourbridge, West Midlands.
Mark (49) na mkewe Denise (57) wamekuwa wakiishi nchi tofauti kwa miaka kadhaa kutokana na majukumu ya kusimamia taaluma za watoto wao. Denise amekuwa akiishi Hispania na Jude, anayekipiga Real Madrid, huku Mark akiishi Ujerumani na Jobe, ambaye anachezea Borussia Dortmund.
Hata hivyo, hivi karibuni mashabiki waligundua mabadiliko baada ya wawili hao kuonekana wakiwa wametengana kwenye mchezo wa Dortmund dhidi ya Athletic Bilbao kila mmoja alikaa kivyake bila kuzungumza. Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti kuwepo kwa hali ya mvutano mkubwa kati yao.
Taarifa zimeibuka kwamba Mark sasa yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi na Punshon, askari wa upelelezi wa West Mercia. Punshon alisambaza picha yake na Mark kwenye ukurasa wake wa Facebook wakiwa pamoja msituni mwezi Agosti, wakiwa na tabasamu na maoni kadhaa ya pongezi kutoka kwa marafiki waliowaandika “Lovely couple xx”.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wa karibu na familia hiyo, mgawanyiko wa wazazi hao umeanza kuwaathiri watoto wao hasa Jobe, ambaye anadaiwa kuwa karibu zaidi na mama yake. Chanzo kutoka Dortmund kimesema:
“Ni wazi Jobe anapitia kipindi kigumu. Hana marafiki wengi, hatoki mara nyingi na muda mwingi anautumia akiwa nyumbani. Mambo ya familia yanaathiri hata kiwango chake uwanjani.”
Wakati huo huo, maisha ya uwanjani kwa ndugu hao yamekuwa magumu pia. Jude, ambaye aling’ara kwenye Euro 2024, hivi karibuni aliondolewa kwenye kikosi cha England cha Thomas Tuchel na kutupwa nje ya kikosi cha kwanza cha Madrid.
Kwa upande wa Jobe, hajawahi kumaliza dakika 90 katika mechi zake 12 za Bundesliga msimu huu.
Mark, ambaye pia ndiye wakala wa watoto wake, alijikuta matatizoni mwezi Agosti baada ya kuripotiwa kujaribu kumkabili kocha wa Dortmund, Nico Kovac, kwa hasira baada ya Jobe kutolewa wakati wa mapumziko kwenye mechi ya kwanza ya msimu. Tukio hilo lilimfanya apigwe marufuku kuingia kwenye vyumba vya wachezaji.
Mark na Denise wamekuwa wakihusishwa moja kwa moja na mafanikio ya watoto wao, wakiwasaidia kupanga mikataba, usajili na kudhibiti fedha zao kupitia kampuni walizoanzisha kwa pamoja. Haijulikani kama utengano huo utaleta mabadiliko katika ushirikiano wao wa kibiashara.
Jude amewahi kusema mara kadhaa kuwa wazazi wake ndio waliomjenga:
“Kabla ya kuwa wazazi bora, wao ni watu bora. Nimejifunza kwa kuwaona jinsi wanavyowaheshimu watu na jinsi wanavyofanya kazi kwa bidii.”
Familia hiyo imekuwa ikiishi maisha ya umbali Denise akiwa Madrid na Jude, huku Mark akiishi na Jobe. Wote wawili wamekuwa wakisafiri mara kwa mara kuhudhuria mechi au hafla kubwa za watoto wao.