
Wikiendi tunayoiendea, wawakilishi wa Tanzania katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ngazi ya klabu, wanakwenda kutupa karata zao muhimu kuwania kuweka mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya makundi, hiyo ni baada ya kutoboa hatua ya awali.
Harakati zilianza na wawakilishi sita wa Tanzania kwa maana ya wanne kutoka Bara na wawili Zanzibar, lakini sasa wamebaki watano baada ya Mlandege kutolewa. Hadi sasa kukiwa na uhakika wa mmoja kucheza makundi.
Hiyo inatokana na kwamba, Azam na KMKM zinakwenda kukutana zenyewe hatua hii upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, yeyote atakayeshinda anacheza hatua ya makundi ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwani kati yao hakuna iliyowahi kufika hapo.
Mtihani unabaki kwa Simba na Yanga upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, sambamba na Singida Black Stars kwa Kombe la Shirikisho Afrika. Hii inaweza kuwa wikiendi ya furaha au lawama. Tusubiri tuone.
Mtihani ni huu
Azam na KMKM zinafahamiana kwa namna moja ama nyingine kwani mara kadhaa zimeshakutana katika mechi tofauti za mashindano na hata kirafiki.
Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho timu hizi zilikutana katika michuano ya Kagame 2021, Azam ilipoteza mara mbili. Ilikuwa Agosti 11, 2021, KMKM ilishinda kwa mabao 3-2 hatua ya makundi, kisha Agosti 14, 2021, Azam ikafungwa tena bao 1-0 kwenye kusaka nafasi ya tatu.
Azam inayonolewa na Kocha Florent Ibenge mwenye rekodi tamu katika michuano ya CAF akiwa na timu tofauti, ndiye aliyebeba tumaini la timu hiyo mbele ya KMKM inayofundishwa na Hababuu Ali Omar.
Pia Azam inaundwa na wachezaji wenye majina makubwa na rekodi nzuri katika mechi za kimataifa, akiwamo Jephte Kitambala, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Issa Fofana na Baraket Hmidi.
KMKM inawategemea nyota wake kadhaa akiwamo Nassor ‘Cholo’ Abdullah, Ahmed Is-haka, Mohammed Hassan, Jumah Khalfan, Abeid Masoud, Mukea Allen, Martin Ather, Mukrim Hassan na Ibrahim Is-haka.
Matamanio ya kila mmoja kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, ndiyo yanaifanya mechi hii kuwa na mvuto wa aina yake.
Hatua ya awali, Azam imeiondosha Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0. Ilishinda mechi zote mbili ugenini na nyumbani kwa mabao 2-0.
Kwa upande wa KMKM, hatua ya awali imeitoa AS Ports ya Djibouti, huku mechi zote mbili zilizochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, imeshinda kwa mabao 2-1, jumla imefuzu kwa ushindi wa 4-2.
Ukiachana na mtihani huo wa ndugu wawili, Singida Black Stars inayokwenda Burundi kukabiliana na Flambeau du Centre, inasaka rekodi.
Rekodi inayosaka Singida Black Stars ni kama ile iliyowekwa na Namungo msimu wa 2020–2021 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi.
Singida Black Stars inafahamu kwamba zipo timu za Tanzania zilizowahi kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo na kushindwa kucheza makundi ambazo ni KMC (2019–2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021–2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025), lakini pia Azam iliyowahi kushiriki mara kadhaa.
Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi, imeitoa Rayon Sports kwa jumla ya mabao 3-1, ilianzia ugenini na kushinda bao 1-0, nyumbani ikashinda tena 2-1. Kwa upande wa Flambeau du Centre imeitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.
Kwa upande wa Flambeau du Centre, ilianza kushiriki mashindano ya kimataifa mwaka 2022, ilianza Ligi ya Mabingwa Afrika na mwaka huu inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika. Hivyo ni mara ya pili kimataifa.
Msimu wa 2022–2023 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, iliishia hatua ya pili ikitolewa na Zamalek kwa jumla ya mabao 6-1. Kabla ya hapo, hatua ya awali iliitoa Al Ittihad ya Libya kwa bao la ugenini baada ya sare ya 2-2.
Simba iliyofundishwa na makocha wawili tofauti akianza Fadlu Davids kisha Hemed Suleiman ‘Morocco’, sasa inakwenda kukabiliana na Nsingizini Hotspurs ikiongozwa na Dimitir Pantev ambaye awali alikuwa Gaborone United, wapinzani walioondolewa na Simba hatua ya awali kwa jumla ya mabao 2-1. Mechi ya kwanza Simba ilishinda ugenini 0-1, nyumbani ikawa sare ya bao 1-1.
Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, itaikaribisha Simba Oktoba 19, mwaka huu, huku timu hiyo msimu uliopita 2024-2025 wakati Simba ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, yenyewe iliishia hatua ya awali ya michuano hiyo ikiondolewa na Stellenbosch kwa jumla ya mabao 8-0, nyumbani ilifungwa 3-0 na ugenini ikachapwa 5-0. Stellenbosch ilipokutana na Simba hatua ya nusu fainali, ikapoteza kwa bao 1-0.
Nsingizini Hotspurs imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Eswatini msimu wa 2024–25.
Yanga imeitoa Wiliete ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0. Imepiga mtu nje ndani ambapo mechi ya kwanza ugenini ilishinda 3-0, nyumbani ikaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0. Imefuzu kwa kishindo bila ya kuruhusu bao kama ilivyo kwa Azam.
Inakwenda kukabiliana na Silver Strikers ya Malawi ambapo mechi ya kwanza ni Jumamosi Oktoba 18, 2025 nchini Malawi.
Yanga inasaka rekodi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo 2023-2024 na 2024-2025 ikiwa chini ya Miguel Gamondi ambaye sasa anainoa Singida Black Stars.
Yanga msimu huu imeshinda mechi nne za mashindano na sare moja kati ya tano ilizocheza, haijaruhusu bao huku ikifunga mabao tisa.