Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Malawi ‘The Flames’, Patrick Mabedi amejiunga na Yanga ambayo ataitumikia katika nafasi ya Kocha Msaidizi.

Kocha huyo anajiunga na Yanga kumsaidia Mjerumani Romain Folz ambaye tayari ameshaiongoza Yanga katika mechi tano za mashindano rasmi msimu huu.

Mabedi ana leseni daraja A ya Ukocha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambayo inamfanya akidhi pia Kocha Mkuu wa timu katika mashindano ya ndani na nje ya Tanzania.

Kocha huyo ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika ambao ameupata akiwa mchezaji na pia kocha.

Amecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini ambako kuanzia 1998 hadi 2006 alikuwa Kaizer Chiefs ambako aliongoza kikosi kama nahodha na kuanzia 2006 hadi 2008 aliitumikia Moroka Swallows.

Kabla ya hapo aliitumikia Bata Bullets ya Malawi kwa muda wa miaka tisa kuanzia 1989 hadi 1998 alipopata fursa ya kujiunga na Kaizer Chiefs.

Mabedi anakuwa Kocha wa pili raia wa Malawi kuinoa Yanga akifuata nyayo za Marehemu Jack Chamangwana ambaye aliwahi kuitumikia timu hiyo na miaka ya nyuma na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2005 na 2006.

Ni kama Yanga imepiga ndege wawili kwa jiwe moja kwani imemchukua Mabedi muda mfupi kabla ya kukabiliana na Silver Striker ya Malawi katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uzoefu wa Mabedi kwa soka la Malawi na wachezaji wake unaweza kuwa faida kwa Yanga katika mechi zake mbili baina ya timu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *