Idadi ya timu tisa zitakazoiwakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 itakamilika leo kwa makundi matatu ambayo bado hayajatoa timu za kufuzu, kukamilisha mchakato huo.

Timu tatu ambazo zitaongoza makundi hayo zitaungana na nyingine sita ambazo zimeshajihakikishia tiketi, kukamilisha idadi ya timu tisa za taifa za Afrika ambazo zinafuzu moja kwa moja kwa fainali za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika mwakani katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Makundi ambayo yanasubiriwa kutoa washindi wa kwenda Kombe la Dunia kutokea Afrika ni Kundi B, Kundi C na Kundi F.

Ushindani wa nafasi moja ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia kundi hilo upo baina ya vinara Senegal wenye pointi 21 na DR Congo walio katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 19.

Senegal inahitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi yake ya nyumbani leo dhidi ya Mauritania ili ifuzu Kombe la Dunia.

Kama itapoteza au kutoka sare, DR Congo inaweza kufuzu ikiwa itaibuka na ushindi kwenye mechi yake ya nyumbani dhidi ya Sudan.

Kuna shughuli pevu kwenye kundi C ambapo timu tatu zilizo juu kwenye msimamo wa kundi hilo, yoyote inawea kufuzu kutegemeana na matokeo ya mechi za leo.

Benin inayoongoza ikiwa na pointi 17, inahitaji ushindi tu ugenini leo dhidi ya Nigeria ili ifuzu Kombe la Dunia.

Nigeria inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 14, inaweza kufuzu ikiwa itapata ushindi wa kuanzia tofauti ya mabao mawili na kuombea Afrika Kusini ipoteze dhidi ya Rwanda.

Afrika Kusini iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 15, itafuzu kama itapata ushindi nyumbani dhidi ya Rwanda na Benin ikapoteza mbele ya Nigeria.

Ivory Coast inayoongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 23, inahitajika kupata ushindi nyumbani dhidi ya Kenya ili itinge Kombe la Dunia mbele ya Gabon iliyo nafasi ya pili ikiwa na pointi 22.

Kama Ivory Coast itapoteza mechi hiyo au kutoka sare, Gabon inaweza kufuzu ikiwa itapata ushindi wa nyumbani dhidi ya Burundi.

Ikumbukwe timu sita tayari zimeshakata tiketi ya kwenda Kombe la Dunia 2026 ambazo ni Ghana, Tunisia, Morocco, Misri, Algeria na Cape Verde.

RATIBA MECHI ZA KUFUZU KOMBE LA DUNIA LEO

Shelisheli vs Gambia (Saa 10:00 jioni)

Afrika Kusini vs Rwanda (Saa 1:00 usiku)

Nigeria vs Benin (Saa 1:00 usiku)

Guinea vs Botswana (Saa 1:00 usiku)

Somalia vs Msumbiji (Saa 1:00 usiku)

Algeria vs Uganda (Saa 1:00 usiku)

DR Congo vs Sudan (Saa 4:00 usiku)

Senegal vs Mauritania (Saa 4:00 usiku)

Morocco vs Congo (Saa 4:00 usiku)

Gabon vs Burundi (Saa 4:00 usiku)

Ivory Coast vs Kenya (Saa 4:00 usiku)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *