Singida. Dk Emmanuel Nchimbi amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kitaendelea kupambana dhidi ya maadui watatu aliowatangaza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya ujinga, maradhi na umaskini kwa nguvu zote.

Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa urais wa CCM amesema hata Rais Samia Suluhu Hassan anaishi na kutenda kwa vitendo ndoto za Mwalimu Nyerere ikiwemo kuwekeza kwenye kilimo.

Mwalimu Nyerere aliyeongoza kupigania Uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania uliopatikana Desemba 9, 1961, aling’atuka madarakani akiwa Rais mwaka 1985 na alifariki dunia Oktoba 14, 1999, London, nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu.

Leo Jumanne, Oktoba 14, ikiwa ni miaka 26 ya kumbukizi ya kifo chake, Dk Nchimbi ametumia mkutano wake wa kampeni za uchaguzi mkuu na kile kinachofanyika kwenye sekta mbalimbali.

Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano uliofanyikia Uwanja wa Kindiko, Wilaya ya Mkalama, Jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida, Dk Nchimbi amesema Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa daima.

Amesema ilani ya uchaguzi mkuu ya chama hicho ya mwaka 2025/2030, imebainisha jinsi inavyokwenda kuendelea kutafuta suluhu ya maadui hao watatu aliowasema Mwalimu Nyerere, Desemba 9, 1961.

Dk Nchimbi amesema ujenzi wa shule, hospitali, mikopo ya asilimia 10 na kuboresha sekta za kilimo na ufungaji ni miongoni mwa mambo yatakayotokomeza maadui hao maradhi, ujinga na umasikini.

“Leo tutafanya kosa kubwa sana kama tukiacha misingi ya umoja, mshikamano na amani kwa nchi yetu huku tukidai tunamuenzi Baba wa Taifa,” amesema Dk Nchimbi huku akiwaomba wananchi uwanjani hapo kupiga makofi kwa urithi huo wa Baba wa Taifa.

Dk Nchimbi amesema katika kipindi chake Mwalimu Nyerere, jambo kubwa alilosimamia kuliko yote ilikuwa kuhakikisha nchi inajitegemea: “Kwa hiyo niwaambieni wana Mkalama, tutafanya kosa kubwa sana kama tutamsahau Baba wa Taifa. Alifanya kazi kubwa kubwa na ya kizalendo.”

Amesema Desemba 9, 1961 siku anatangaza Uhuru wa Tanganyika, miongoni mwa mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliliambia Taifa ni kutangaza maadui wakuu wa nchi ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Amesema Rais Samia naye ameendelea kupambana na maadui hao kwa kuanzisha miradi mbalimbali katika kila eneo la nchini ikiwemo za afya ili suala la maradhi lipate suluhu, ujinga kwa kujenga shule na kuboresha mifumo ya elimu na umaskini kwa kufungua fursa za kiuchumi.

“Hapa Mkalama, miaka mitano ijayo tunakwenda kuiboresha Hospitali yetu ya wilaya ili iwe ya kisasa itakayotoa huduma zote muhimu, lakini tutajenga vituo vipya vya afya vitano, kuongeza zahanati nane, kujenga vyumba za watumishi wa afya 12. Mpango wa elimu mpya kuanzia chekechea hadi kidato cha sita itaongezwa ili adui maradhi na ujinga tuendelee kumtokomeza,” amesema
 

Majimbo matatu, kata 101

Akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Singida, Martha Mlata amesema kama chopa imetua hapa, barabara itashindikana kweli kujengwa?

Dk Nchimbi ametumia usafiri wa helikopta kutoka Dodoma hadi Iramba, karibu na eneo ulipofanyika mkutano huo.

Mlata amesema mkoa huo una majimbo manane na kati yake wanawake wawili wamepitishwa na chama kugombea kwenye majimbo.

“Kati ya majimbo haya manane matatu hayajapata upinzani lakini hata yale yaliyopata wapinzani, wapinzani wenyewe kwangu pakavu tia chumvi, hawatusumbui.

“Tuna kata 136 mkoani Singida, kati ya hizi ni kata 35 tu ndio tumepingwa na waliotupinga bado wamelala hatujui wapo wapi. Pamoja na kata chache na majimbo tunaendelea kutafuta kura ili ushindi uwe mkubwa sana,” amesema Mlata.

Hii ina maana kwamba majimbo matatu na kata 101 zitapigwa kura za ndio au hapana kwa wagombea.
 

Alicholisema Kishoa, Pareso

Mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Jesca Kishoa amesema tarehe hiihii tukiwa tunamuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ni heshima kubwa kumpokea Dk Nchimbi wilayani humo.

“Nikimwona Rais Samia na Dk Nchimbi namwona Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ndani yao,” amesema Kishoa.

Kishoa amesema miaka minne ya Rais Samia: “Ameleta mabilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo kwenye nyanja mbalimbali.”

Hata hivyo, Kishoa ambaye amekuwa mbunge wa viti maalumu kwa miaka 10 kupitia Chadema amesema, wananchi wa Iramba wamesema watakwenda kupiga kura ila wanataka barabara ya kutoka Iguguno hadi Simiyu ya kilomita 89 wanaomba ifanyiwe kazi.

Amesema kati ya vitongoji 388 vilivyopo, 90 havina umeme, lakini wamegusia suala la elimu, afya, skimu za umwagiliaji yafanyiwe kazi.

“Nimejipanga kuwatumikia, hii ni saizi yangu sana ubunge na ninawahakikishia mkinipeleka bungeni, hampeleki mtoto, najua uchochoro wote, nimekaa bungeni miaka 10 najua kila njia,” amesema Kishoa.

Kada wa CCM, Cecilia Pareso amesema chama hicho kimejiandaa kushinda kwa sababu kimeteua wagombea wazuri akiwemo Samia na msaidizi wake, Dk Nchimbi.

“Katika kipindi cha uongozi wa Samia, amefanya maendeleo makubwa kuanzia kwenye vijiji, kata na Taifa. Amedhihirisha kwamba kina mama wakipewa nafasi, Taifa linainuka na kusonga mbele,” amesema Pareso aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema.

Pareso amesema: “Kura yako moja ndiyo uhakika wa upatikanaji wa maji, elimu, barabara, mbolea, huduma bora za afya katika maeneo yako lakini ndiyo itakayotupa Serikali itakayokwenda kutekeleza ilani ya kazi na utu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *