Manchester, England. Sio siri Phil Foden alikuwa kwenye kiwango bora kabisa Manchester City ilipofanya kweli kwenye msimu wa 2023-24.

Kiungo huyo mshambuliaji, ambaye anaweza pia kucheza kwenye wingi zote, kushoto na kulia, alikuwa katika kiwango matata sana wakati Man City iliponyakua taji lake la nne mfululizo la Ligi Kuu England.

Alistahili kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu England kutokana na kiwango chake bora kabisa kwa msimu huo.

Kwa mchezaji anayecheza kwenye nafasi kama ya Foden kwa kawaida amekuwa akivaa jezi Namba 10 au 11 kwenye klabu zao, lakini mambo yamekuwa tofauti kabisa kwani staa huyo, amegoma kubadilisha jezi Namba 47.

Kuna sababu zilizomfanya Foden, ambaye ni mchezaji kijana kuwahi kushinda taji la Ligi Kuu England, alipofanya hivyo akiwa na umri wa miaka 17 na siku 350.

FODE 02

KWA NINI FODEN ANAVAA NAMBA 47?

Kinachoelezwa ni Foden alipewa ofa ya kuchukua Namba 10 wakati mchezaji Sergio Aguero alipoondoka Man City mwaka 2021.

Hata hivyo, licha ya kupata nafasi hiyo ya kurithi mikoba ya straika huyo matata kabisa kwa mabao, Foden hakushawishika kuchukua jezi Namba 10.

Aliamua kubaki na Namba 47, ambayo imekuwa na kumbukumbu ya kipekee katika maisha yake. Foden anavaa Namba 47, ikiwa ni kumbukumbu mahususi kwa marehemu babu yake, Ronnie, ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 47.

Kutokana na kutaka kuwa na kumbukumbu hiyo ya babu yake Ronnie, Foden amechagua kuvaa jezi hiyo yenye Namba 47 kwenye kila mechi anayotumikia klabu yake. Na kama utaratibu wa kutumia Namba 47 ungetumika kwenye soka la kitaifa, basi Foden angetumia jezi hiyo kwenye kikosi cha Three Lions. Kingine ni Ronnie alikuwa shabiki mkubwa wa Man City.

Kama ilivyo kwa Trent Alexander-Arnold, aliyekuwa akivaa jezi Namba 66 kwenye kikosi cha Liverpool, Foden ameng’ang’ana kwenye Namba 47.

FODE 01

FODEN ANA TATTOO YA NAMBA 47

Anapokuwa kwenye soka la kimataifa, Foden haonekani kuwa na Namba 47 kwenye jezi yake, lakini kuonyesha namba hiyo anakuwa nayo muda wote, ameamua kujichora tattoo shingoni nyuma ya sikio yenye namba hiyo.

Hiyo ina maana, Namba 47 itaambatana na Foden kila mahali, iwe uwanjani au kitandani akiwa amelala na hata atakapostaafu soka, ataendelea kubaki na Namba 47 kwenye mwili wake.

Hata hivyo, tattoo ya Namba 47 si mchoro pekee uliopo kwenye mwili wa Foden, ambapo upande wa pili wa shingo yake kuna tatoo nyingine ya maneno, inayosomeka: “Sky is the limit.”

Akiwa kwenye umri mdogo, Foden kwenye kabati lake la mataji, tayari amebeba ya kutosha, ikiwamo Ligi Kuu England mara sita, ikiwa ni sehemu tu ya mataji kibao aliyobeba ikiwamo UEFA Champions League,  European Super Cup na Club World Cup.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *