Azam FC imekuwa klabu ya kwanza Tanzania kuitikia wito wa kujiunga na Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA) uliotolewa leo, Jumanne, Oktoba 14, Dar es Salaam na mwenyekiti wake Hersi Said.
Hersi ambaye pia ni Rais wa Yanga, amezisihi klabu za soka Tanzania za Ligi Kuu na Ligi ya Championship kujiunga na Chama hicho akisema kina manufaa makubwa kwao.

“Changamoto ni kubwa kwa sababu taasisi imezaliwa mikononi mwetu. Tunaiendesha katika njia ambayo ni salama zaidi. Tulikuwa na changamoto ambazo tumeshaziweka sawa.
“Jana tulikuwa na mkutano wa bodi ya ACA na tumeweza kupitisha usajili wa klabu kwa hiyo fomu zipo tayari kwa klabu zote. Ambavyo viko Tanzania na Afrika kwa ujumla kuanza kuwa wanachama wa ACA. Fomu ziko tayari, ada ya usajili ni Dola 1,000 (Sh2.5 milioni) kwa mwaka.
“Klabu italipa Dola 1,000 na itakuwa mwanachama wa ACA na kuna maslahi makubwa ya klabu kuwa sehemu ya umoja huo,” amesema Hersi.

Makamu wa Rais wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’ amesema kuwa klabu yake imeona umuhimu mkubwa wa ACA na imejipanga kujiunga haraka iwezekanavyo.
“Injinia amezungumza hapa mapema kwamba msimu huu ambao tunashiriki wameanza kuongeza na itaongezeka. Niwe shuhuda pia tarehe 16, mwezi wa tisa tumeshapokea pia Dola 100,000 (Sh245 milioni).
“Kwa hiyo hizo ndio fursa ambazo sisi kama Azam FC tumeshaanza kunufaika nazo. Lakini pia amezungumza jambo ambalo sikuwa na taarifa nalo ya kwamba fomu zimeanza kutoka kwa klabu zinazotaka kujiunga.
“Sisi kama Azam FC, mimi kwa niaba ya Azam FC, tutakuwa watu wa mwanzo kuchukua fomu na tutalipia na kujiunga na African Club Association,” amesema Popat.