Tarime. Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuibua na kuandika habari za vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na vile wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu, ili kusaidia mamlaka husika kuchukua hatua zitakazosaidia makundi hayo kuwa salama.

Ombi hilo limetolewa mjini Tarime leo Oktoba 14, 2025 na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Sylivester alipokuwa akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya namna ya kuandika habari za ukatili wa kijinsia, kwa kuzingatia haki za binadamu kwa makundi yanayofanyiwa vitendo hivyo.

Siwema amesema licha ya jitihada zinazofanywa na wadau pamoja na Serikali katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake watoto na watu wenye ulemavu, bado vitendo hivyo vimeendelea kutokea katika jamii, jambo ambalo linahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa kila mdau katika kupambana nalo.

Ofisa kutoka Muungano wa Vilabu vya Waandishi Tanzania (UTPC), Victor Maleko akitoa mafunzo kwa Waandishi wa habari kuhusu uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia. Picha na Beldina

“Takwimu zinaonyesha kupungua kwa vitendo vya ukatili lakini bado tatizo lipo na matukio mengine yanafanywa kwa siri kubwa, niwaombe waandishi kwa kutumia taaluma zenu, ingieni huko nendeni hadi vijijini mkaibue haya matukio yanayofichwa, hii itasaidia Serikali na wadau wengine kuchukua hatua,” amesema.

Amesema waandishi wa habari ni sehemu ya jamii, hivyo wana wajibu wa kulinda na kuhakikisha kuna kuwepo na ustawi wa jamii hasa watoto wa kike na watu wenye ulemavu na kwamba ustawi huo utakuwepo pale makundi hayo yatakapopata haki sawa kama ilivyo kwa watu wengine.

Amesema ukatili wa kijinsia ni kikwazo cha maendeleo na ustawi wa wanawake nchini hivyo kuna kila sababu ya kula mdau kushiriki katika mapambano hayo.

Mratibu wa miradi katika shirika lisilokuwa la kiserikali linalishughulikia haki za watoto la C-Sema, Michael Marwa amesema shirika lake limeandaa mafunzo hayo kwa waandishi ili kufanya majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, hatua itakayosaidia jamii kunufaika zaidi na taaluma hiyo ya habari.

“Shirika la C-Sema limewakutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya mafunzo rejea kuwakumbusha kuzingatia misingi ya uandishi wakati wa kuripoti matukio ya manusura wa ukatili, hii ikiwa ni moja ya mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii,” amesema.

Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa kwenye mafunzo kuhusu uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia.  Picha na Beldina Nyakeke

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwakumbusha waandishi wa habari juu ya misingi ya haki za binadamu sambamba na haki za waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo wakati waandishi hao wanapotimiza majukumu yao wasisahau kuhusu misingi hiyo.

 “Kuna vitendo vinafanyika katika jamii zetu ambavyo wakati mwingine huwa vinatokana na ukosefu tu wa elimu, hivyo sisi waandishi tuna jukumu la kutoa elimu kupitia vyombo vyetu ili jamii ielewe madhara ya vitendo hivyo na kuachana navyo,” amesema Paschal Malulu.

Helena Magabe amesema mafunzo hayo yatawasaidia waandishi wa habari kufanya kazi zao bila kuvunja haki za binadamu hasa waathirika wa vitendo hivyo, kwa maelezo kuwa kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya namna ya kuandika habari kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, wapo waandishi ambao wamekuwa wakienenda tofauti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *