Miaka kadhaa baadaye katika kitabu alichoandika kuhusu maisha yake ya siasa alikiri kuhusika katika jaribio hilo la mapinduzi kwa kiasi kikubwa.
Baadhi ya wanasiasa walitaka ashtakiwe tena kwa uhaini ila kisheria muda wa mashtaka kuanzishwa tena ulikuwa umepita.
Miongoni mwa waliofungwa pamoja naye wakati wa harakati zake za kutaka demokrasia ni wanasiasa Kenneth Matiba na aliyekuwa meya wa jiji la Nairobi Charles Rubia.
Raila Odinga alirejea nchini Kenya mwaka 1992 wakati huo akijiunga na chama alichokianzishwa baba yake Jaramogi Oginga Odinga, FORD na ndiyo mwaka ambapo uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulifanyika nchini Kenya.
Raila alishinda ubunge wa jimbo la Langata, lakini baba yake hakufanikiwa kushinda urais dhidi ya Daniel arap Moi.