
Rais wa Marekani ametangaza siku ya Jumapili, Oktoba 19, mwisho wa msaada wa kifedha wa Marekani kwa Bogota, akimshutumu mwenzake wa Colombia, Gustavo Petro, kwa kushindwa kukabiliana na biashara ya madawa ya kulevya nchini mwake.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kama kawaida, tangazo limekuja kwa njia ya chapisho kwa herufi kubwa kwenye kukwaa la Truth Social. “KUANZIA LEO, MALIPO HAYA, AU AINA NYINGINE YOYOTE YA MALIPO AU MISAADA, HAITAFANYIKA TENA” kwa Colombia, Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, bila kutaja ni msaada gani alikuwa akimaanisha. Gustavo Petro “hafanyi lolote kukomesha” uzalishaji wa madawa ya kulevya, rais wa Marekani ameongeza, akimshutumu mwenzake wa Colombia kuwa “kiongozi wa biashara haramu wa dawa za kulevya ambaye anahimiza sana uzalishaji mkubwa wa mihadarati” nchini mwake.
Mshtumiwa, akibaini kuwa rais wa Marekani “anadanganywa” na “washauri” wake. “Ninapendekeza Trump aichunguze kwa makini Colombia na kubaini wapi wafanyabiashara wa dawa za kulevya wako na wapi wako wanademokrasia,” amejibu kwenye mtandao wa kijamii wa X. “Ninaheshimu historia, utamaduni na raia wa Marekani. Wao si maadui zangu (…) Tatizo ni Trump, si Marekani,” Gustavo Petro amebainisha.
Dola milioni 740 za msaada mnamo mwaka 2023
Colombia ndio nchi ya Amerika Kusini inayopokea msaada mkubwa zaidi wa kifedha kutoka Washington, kulingana na data ya serikali ya Marekani, kwa zaidi ya dola milioni 740 zililipwa mnamo mwaka 2023, mwaka wa hivi karibuni ambapo data kamili zinapatikana. Nusu ya fedha hizi zilitengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Zingine zinaunga mkono programu za kibinadamu na chakula, miongoni mwa mambo mengine.
Hadi mwezi Septemba, Bogota ilichukuliwa kuwa mmoja wa washirika 20 wa Marekani wa kupambana na dawa za kulevya, na kuiruhusu kudai malipo makubwa ya kifedha. Lakini Ikulu ya White House ilibatilisha hadhi hii, ikitoa mfano wa “rekodi” ya utengenezaji wa kokaini na “majaribio yaliyofeli” katika mazungumzo na “makundi ya kigaidi yanayojihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya.”
Colombia ndiyo inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa kokeini, ikiwa na rekodi ya tani 2,600 mwaka 2023, 53% zaidi ya mwaka uliopita, kulingana na Umoja wa Mataifa (UN). Lakini Gustavo Petro pia anadai kuwa uzalishaji wa kokeini umepungua chini ya serikali yake na kwamba makadirio ya Umoja wa Mataifa yanaleta matatizo ya kimbinu.
Tangu aingie madarakani mwaka wa 2022, rais wa Colombia ameendesha mabadiliko ya dhana katika vita vinavyoongozwa na Marekani dhidi ya dawa za kulevya, akilenga kukabiliana na matatizo ya kijamii yanayochochea biaashara ya dawa za kulevya. “Adui mkuu wa biahara ya dawa za kulevya nchini Colombia (…) ndiye aliyefichua uhusiano wake na mamlaka ya kisiasa ya Colombia. Huyo alikuwa mimi,” kiongozi huyo amebainisha.
Kusitishwa kwa misaada ya kifedha ya Marekani kunaashiria hatua ya mabadiliko katika uhusiano ambao ulianza zaidi ya miaka ishirini iliyopita, uliozaliwa nje ya Plan Colombia iliyozinduliwa mwaka 2000-ushirikiano wa kimkakati ambapo Washington iliwekeza zaidi ya dola bilioni 10 kusaidia vita dhidi ya madawa ya kulevya na usalama wa nchi.
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili, washirika wa kihistoria, ulifikia kiwango cha chini kabisa baada ya kuingia madarakani kwa Donald Trump na rais wa kwanza wa mrengo wa kushoto katika historia ya Colombia. Vita vya maneneo kati ya watu hao wawili vimejitokeza tangu Marekani ilipoanzisha mashambulizi ya kijeshi katika visiwa vya Caribbean, huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye boti zinazoshukiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Rais wa kwanza wa mrengo wa kushoto katika historia ya Colombia anaishutumu Washington kwa kukiuka mamlaka ya maji ya kitaifa na kumuua mvuvi mmoja wakati wa moja ya mashambulizi haya.