
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ameitaka Israel kutekeleza kwa haraka uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), akisisitiza wajibu wa utawala huo chini ya sheria za kimataifa kuhakikisha misaada muhimu inafika Gaza na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Turk alisisitiza kuwa maoni ya ushauri ya ICJ yamethibitisha tena kuwa sheria za haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa zinatumika katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa. Uamuzi huo unaitaka Israel “kuheshimu, kulinda, na kutekeleza” haki za binadamu za Wapalestina, ikiwemo upatikanaji wa misaada ya kuokoa maisha.
Uamuzi wa ICJ uliotolewa Jumatano ulieleza wazi wajibu wa Israel chini ya Mkataba wa Geneva kusaidia juhudi za misaada zinazofanywa na mashirika huru ya kibinadamu kama Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na shirika la UN la wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Mahakama hiyo ilisisitiza haki za msingi kama haki ya kuishi, uhuru dhidi ya mateso, usalama, uhuru wa kutembea, ulinzi wa familia, viwango vya maisha vinavyokubalika, afya, elimu, kutobaguliwa, na haki ya kujitawala.
Turk aliwahimiza wahusika wote kuweka mbele uhai wa watu na kuhakikisha msaada muhimu unafika Gaza, akieleza kuwa hilo ni “hatua ya kwanza kuelekea urejeshaji na ujenzi wa amani unaojikita katika haki za binadamu.” Aliongeza kuwa kutii uamuzi huo ni muhimu ili kupunguza janga la kibinadamu na kusaidia mkataba wa kusitisha mapigano kugeuka kuwa amani ya kudumu.
“Mataifa yote yanapaswa kuchukua hatua haraka kukabiliana na hali ya kutisha ya haki za binadamu na kibinadamu inayoshuhudiwa kwa sasa,” alisema Turk, akitoa wito wa kuletwa kwa msaada wa haraka Gaza ili kufungua njia ya uthabiti wa muda mrefu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Mnamo Julai 2024, ICJ ilitoa maoni ya ushauri ikisema kuwa ukaliaji wa maeneo ya Palestina na Israel ni “haramu” na lazima ukome haraka iwezekanavyo. Katika maoni mengine ya ushauri yaliyotolewa Jumatano, mahakama hiyo ya Hague ilisema kuwa Israel, kama utawala unaokalia kwa mabavu, una wajibu wa kushirikiana na mashirika ya UN kurahisisha misaada ya kibinadamu kwa Gaza. Mahakama hiyo imekemea vikali kizuizi cha kibinadamu kinachotekelezwa na utawala wa Israel katikati ya vita vinavyotajwa kuwa vya mauaji ya halaiki.
Mahakama pia ilisema kuwa Israel haikuweza kuthibitisha madai yake kwamba UNRWA inapendelea upande mmoja au kwamba idadi kubwa ya wafanyakazi wake ni wanachama wa Hamas au makundi mengine ya kupigania ukombozi wa Palestina. Maoni hayo yaliombwa na Baraza Kuu la UN mnamo Desemba 2024 baada ya Israel kuzuia UNRWA kuendeleza shughuli zake, jambo lililopunguza sana uwezo wake wa kufikisha msaada Gaza.