Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani, amesisitiza kuwa mashinikizo la kiuchumi kutoka mataifa ya Magharibi hayawezi kuathiri uthabiti wa taifa.

Akizungumza kwa msisitizo maalum, Larijani alisema: “Magharibi inadhani kuwa kwa kutumia mashinikizo ya kiuchumi inaweza kudhoofisha uimara wa Iran. Lakini taifa hili, likiwa na imani na msimamo thabiti, litavuka kipindi hiki pia.”

Larijani alifafanua juhudi za Tehran za kuzuia utekelezaji wa kile kinachojulikana kama snapback mechanism—utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Alifichua kuwa baadhi ya madola ya Magharibi yalitaka Iran ipunguze uwezo wa makombora yake hadi chini ya kilomita 500, akilitaja hilo kama jaribio la kuondoa silaha muhimu ya kujihami ya taifa la Iran.

Iran imekataa uhalali wa hatua ya mataifa ya E3—Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza—kuanzisha tena vikwazo hivyo, ikitaja hatua hiyo kuwa batili. Jumamosi iliyopita, Tehran ilitangaza kumalizika kwa kipindi cha miaka 10 cha Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2231, ambalo lilikuwa likizuia baadhi ya vipengele vya mpango wa nyuklia wa Iran.

Katika kumbukumbu ya shahidi Hossein Hamedani, kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) aliyeuawa katika vita dhidi ya kundi la Daesh nchini Syria, Larijani alieleza kuwa Iran ilifanya uamuzi sahihi wa kupambana na ugaidi nje ya mipaka yake.

Alisema: “Wengine hujiuliza kwa nini tulitoa mashahidi wengi na kugharimika sana, ilhali ukanda bado una mgogoro. Ukweli ni kwamba magaidi wa Daesh walikuwa viumbe hatari waliolenga kuleta machafuko ndani ya Iran.”

Larijani alisisitiza kuwa kundi hilo la kigaidi lilianzishwa na Marekani, lakini likadhoofishwa kupitia mikakati ya kiusalama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *