Gilles Carbonnier, Makamu wa Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), ameelezea masikitiko yake kuhusu uwepo wa zaidi ya migogoro 50 inayoendelea barani Afrika, ikiwakilisha takriban 40% ya migogoro ya silaha duniani.

Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa, Carbonnier amesema kwamba kinachotia wasiwasi sana ni kwamba idadi ya migogoro ya silaha barani Afrika imeongezeka kwa 45% tangu 2020.

Ameongeza kuwa zaidi ya migogoro 50 hai ya silaha barani Afrika, inayowakilisha takriban 40% ya migogoro yote duniani, imesababisha watu takriban milioni 35 barani humo kuwa wakimbizi, yaani karibu nusu ya idadi ya wakimbizi wote duniani.

Makamu wa Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu amesema hali hiyo inatia wasiwasi hasa nchini Sudan, ambayo imekumbwa na vita vya umwagaji damu tangu Aprili 2023.

Miigogoro imelazimisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi Afrika

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yameua makumi ya maelfu ya watu, kuwafanya wakimbizi takriban milioni 12, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekielezea kuwa ni “mgogoro mbaya zaidi wa binadamu duniani.”

Pia ameelezea masikitiko yake kutokana na kuanza tena vitendo vya kihasama nchini Somalia na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo vurugu zimeongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku kundi la M23 likidhibiti miji mikubwa ya Goma na Bukavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *