
Russia imelaani vikali vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya makampuni yake makubwa ya mafuta, ikionya kuwa hatua hizo za Washington zinaweza kuisukuma dunia kuelekea hali ya kutokuwa na utulivu.
Mnamo Oktoba 23, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, alisema kuwa hatua hizo za adhabu dhidi ya sekta ya nishati ya Russia zitakuwa na athari mbaya kwa walioweka vikwazo, akisisitiza kuwa Moscow haitakubali kuhatarisha maslahi yake ya kitaifa. Alieleza kuwa hatua hiyo ni “isiyo na tija kabisa,” na kuongeza kuwa Russia “imejijengea kinga madhubuti dhidi ya vikwazo vya Magharibi” na itaendelea kuimarisha sekta yake ya nishati licha ya shinikizo la kiuchumi.
Zakharova pia alisisitiza kuwa Moscow iko tayari kwa mazungumzo, akisema hakuna “vikwazo vikubwa” vinavyokwamisha mazungumzo ya amani, mradi tu yatajengwa juu ya “heshima ya pande zote na uhalisia.”
Kwa upande mwingine, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, alikemea vikwazo hivyo katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi, akisema kuwa Beijing inapinga hatua za upande mmoja zisizo na “msingi wa sheria za kimataifa au idhini ya Umoja wa Mataifa.” Alisisitiza kuwa “mazungumzo na majadiliano ndiyo njia pekee ya kutatua mgogoro wa Ukraine, si shinikizo na vitisho.”
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulitangaza vikwazo hivyo Jumatano, vikilenga Rosneft na Lukoil—makampuni mawili makubwa ya mafuta ya Russia—kwa kile Washington ilichokiita “msimamo wa Moscow wa kukataa kumaliza vita vya Ukraine.”
Vikwazo hivyo pia vinahusisha makampuni tanzu kadhaa yanayohusiana na Rosneft na Lukoil.
Aidha, vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya hatua kwa hatua ya uagizaji wa gesi ya LNG kutoka Russia na masharti mapya dhidi ya meli za kubeba mafuta za Moscow.
Hatua hizo zinawakilisha hatua ya kwanza ya Rais Trump kuhusu Ukraine katika muhula wake wa pili, na zimesababisha bei ya mafuta kupanda kwa zaidi ya dola mbili kwa pipa.
Siku hiyo hiyo, Umoja wa Ulaya uliidhinisha kifurushi kipya cha vikwazo, kufuatia hatua ya Uingereza ya kuviwekea vikwazo Rosneft na Lukoil mnamo Oktoba 16.
Mnamo Oktoba 21, Rais Trump alifuta mkutano uliopangwa na Rais wa Russia Vladimir Putin, akieleza kuwa mazungumzo hayo ni “kupoteza muda.”
Uamuzi huo dhidi ya Russia unaashiria mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani kuelekea taifa hilo kubwa la Ulaya, kwani awali Rais Trump alikuwa amechukua mkondo wa kidiplomasia kuelekea Moscow.