Afisa wa taasisi ya Humanity and Inclusion amesema kazi ya kukusanya silaha ambazo hazijalipuka katika Ukanda wa Gaza inaweza kuchukua kipindi cha miaka 20 hadi 30, akilitaja eneo hilo kama “uwanja wazi wa mabomu.”
“Kuondolewa kabisa vifusi hakutatokea kamwe kwa sababu viko chini ya ardhi. Bado vitaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo,” amesema Nick Orr, mtaalamu wa kukusanya silaha za milipuko katika shirika hilo, akilinganisha hali hiyo na kile kilichotokea katika miji ya Uingereza baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Orr, ambaye alitembelea Gaza mara kadhaa wakati wa vita, ni sehemu ya timu ya watu saba kutoka taasisi ya Humanity and Inclusion ambayo imepangwa kuanza kutafuta mabaki zana za vita ndani ya miundombinu muhimu, kama vile hospitali na maeneo ya kuokea mikate, wiki ijayo.

Hata hivyo, Orr ameeleza kwamba mashirika ya misaada, ikiwa ni pamoja na shirika lake, bado hayajapewa ruhusa kamili kutoka Israel ya kuanza kuondoa au kuharibu silaha ambazo hazijalipuka, au kurejesha vifaa muhimu.
Hifadhidata ya Umoja wa Mataifa imeonyesha kuwa zaidi ya watu 53 wameuawa na mamia kujeruhiwa kutokana na mabaki ya vita vya miaka miwili vya kuangamiza watu vilivyoanzishwa na Israel huko Gaza, huku mashirika ya misaada ya kibinadamu yakiamini kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia mabomu ya kutegwa ardhini (UNMAS), Luke Irving, alionya wiki iliyopita kwamba hatari ya silaha ambazo hazijalipuka katika Ukanda wa Gaza inaongezeka baada ya kusitisha mapigano.