
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali muswada uliopasishwa katika Bunge la Israel (Knesset) wa kunyang’anywa eneo la Ukingo wa Magharibi huko Palestina ukiutaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa hati na kanuni za Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei alitoa matamshi hayo jana Alkhamisi, siku moja baada ya Bunge la Israel kupiga kura ya kuunga mkono muswada ambao utatekeleza sheria ya utawala huo ghasibu katika vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi, pamoja na muswada mwingine unaoidhinisha kunyakuliwa eneo la Maale Adumim. Miswada hiyo lazima ipigiwe kura tatu za ziada katika plenum ili kugeuka kuwa sheria.
Baqaei amesema kwamba muswada huo ni hatua nyingine katika njia ya upanuzi wa kikoloni na kihalifu wa utawala huo, ambao unaendelea kwa miongo minane ya ukiukaji endelevu wa haki za msingi za kujitawala za watu wa Palestina.
Ameongeza kuwa sera hizi zilizopitishwa na Israel zinathibitisha mpango wa utawala huo wa kuangamiza kizazi katika ardhi yote inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Baqaei pia ameangazia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu unaoendelea kufanyika Ukingo wa Magharibi na mauaji ya kimbari huko Gaza. Amesema ni jukumu la nchi zote kuchukua hatua madhubuti za kuzuia kuangamizwa Palestina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito kwa nchi za Kiislamu na jamii ya kimataifa kuchukuliwa hatua za haraka na kuzuia ukiukwaji wa wazi wa haki za kihistoria za watu wa Palestina.
Itakumbukwa kkuwa, mnamo Julai 2024, ICJ ilitoa maoni ya ushauri ikisema kwamba uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria na lazima ukomeshwe haraka iwezekanavyo.