
Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitiza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ni gaidi, na iwapo dunia inataka kumtambua gaidi halisi, basi mtu huyo si mwingine bali ni Trump mwenyewe.
Kwa mujibu wa shirika la habari ISNA, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami , Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran — katika hotuba yake ya kisiasa ya Ijumaa ya leo ameashiria kauli za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati wa kikao na mabingwa wa michezo mbalimbali na washindi wa medali za kimataifa na kusema: “Maelekezo ya Kiongozi yalikuwa na vipengele viwili muhimu. Kipengele cha kwanza kilikuwa ‘Tumaini’. Alisema kwamba Iran na vijana wake ni mfano wa matumaini. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, nchi yetu ipo katika nafasi ya juu duniani katika tafiti za sayansi na teknolojia kama vile sayansi ya nano laser, nyuklia, sekta za kijeshi na tiba. Haya yote ni chanzo cha matumaini. Amekuwa akisema mara nyingi kwamba mustakabali wa Iran ni ang’avu zaidi kuliko jana, na kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’an, tumaini ni msingi wa ukuaji na ustawi wa taifa.”
Ameongeza kuwa kipengele cha pili katika maelekezo hayo kilihusu “Heshima na Uwezo wa Taifa.”
“Kiongozi Muadhamu alifichua uongo wa Trump. Trump anadai kwa uongo kuwa anapigana na ugaidi, ilhali vita vya Gaza vimeonyesha wazi kuwa si utawala wa Kizayuni tu uliokuwa nyuma ya mauaji, bali ni serikali ya Marekani yenyewe. Wameua zaidi ya watoto elfu ishirini, na katika kipindi cha miaka miwili wameua takriban watu elfu sabini. Hapa Iran pia waliwaua mashahidi wetu zaidi ya elfu moja, wakiwemo watoto wachanga na wanawake wasio na hatia.”
Imamu huyo wa muda wa Ijumaa amesisitiza kwamba:
“Trump ndiye gaidi. Iwapo dunia itataka kumbaini gaidi wa kweli, basi huyo ni Trump mwenyewe. Trump alikiri kuwa ndiye aliyehusika na mauaji ya Shahidi Qassem Soleimani na pia mashahidi wetu wa nyuklia kama Toharanchi na Abbasi. Trump ni gaidi na mlezi wa magaidi, na madai yake ya kupambana na ugaidi ni uongo mtupu.”
Aliongeza kuwa Trump pia anahadaa kuwa rafiki wa wananchi wa Iran, ilhali tangu mapinduzi ya tarehe 28 Mordad 1332 (1953) hadi leo , zaidi ya miaka sabini , Wamarekani wamehusika na uhalifu mwingi nchini Iran, wakiunda utawala wa kifashisti na wa kinyama wa kifalme wa Pahlavi.
Ameendelea kwa kuhoji hivi: “Je, hawa wanaweza kuitwa marafiki wa wananchi?
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema ubalozi wa Marekani ulitumika kitovu cha njama dhidi ya taifa la Iran. Ameendelea kwa kusema: “Kwa mtazamo wao, yeyote anayepinga uovu wao huitwa gaidi — iwe ni Hizbullah ya Lebanon, Ansarullah ya Yemen, Hashd al-Sha’abi ya Iraq, au Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Lakini kwa mtazamo wa mataifa huru na yenye utu, makundi haya yanaheshimiwa kwa kusimama imara dhidi ya dhulma na uovu wa Marekani.”