Jeshi la Nigeria limetangaza kwamba limewaua wanamgambo 50 waliokuwa wakiendesha shughuli zao katika makundi yenye msimamo mkali ambao walikuwa wametumia ndege zisizo na rubani kufanya mashambulizi kadhaa kwenye kambi za kijeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi imesema, “Vikosi vya Jeshi, vikisaidiwa na ndege za kivita, vimehusika katika mashambulizi yaliyoratibiwa asubuhi ya jana Alkhamisi dhidi ya waasi walioanzisha mashambulizi kwenye kambi za jeshi katika maeneo ya Dikwa, Mafa, na Gajebu katika Jimbo la Borno, na pia huko Katarko katika Jimbo jirani la Yobe.”

Jeshi la Nigeria halijatambua kundi lililohusika na mashambulizi hayo, lakini Shirika la Habari la Ufaransa limenukuu vyanzo vya kijasusi vikisema kwamba wahusika ni wa wapiganaji wa kundi la Daesh Magharibi mwa Afrika.

Kanali Sani Uba amesema: “Juhudi za pamoja za nchi kavu na angani zimepelekea kuangamizwa magaidi zaidi ya 50 katika maeneo yote. Operesheni za nchi kavu na angani bado zinaendelea kuwasaka “waasi zaidi ya 700 waliojeruhiwa.” 

Jeshi la Nigeria limekuwa likipigana vita vya miaka 16 dhidi ya kundi la Boko Haram na tawi la Daesh Magharibi mwa Afrika (ISWAP).

Shirika la Habari la Ufaransa linasema, mzozo huo umesababisha mauaji ya zaidi ya watu 40,000 na kuwalazimisha wengine wapatao milioni mbili kuwa wakimbiizi kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *