Israel inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa katika historia yake. Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala wa Kizayuni, alikiri hivi karibuni katika kikao cha kamati moja ya Knesset kwamba Israel hivi sasa iko katika mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa katika historia yake.

Alisema: “Nchi 142 zimelitambua taifa la Palestina, na Mfuko wa Utajiri wa Norway umeondoa uwekezaji wake Israel. Makampuni ya kimataifa yamejiondoa katika miradi ya Israel, na huko Ulaya nako, wamiliki wa maduka madogo wanaondoa kimya kimya bidhaa za Israel kwenye rafu za maduka yao.”

Israel iko katika hali mbaya ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, na inajikuta kati ya kuanguka kisiasa, kutengwa kiuchumi na mgawanyiko mkubwa wa kijamii. Kukiri Yair Lapid, kiongozi wa upinzani kwenye Knesset, kwamba Israel inasumbuliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa katika historia yake, hakuelezei hali ya muda tu, bali ni taswira ya ukweli mchungu na muundo ambao unadhoofisha mfumo wa Tel Aviv kutokea ndani.

Yair Lapid

Kando na hayo, data rasmi zilizochapishwa na Kituo cha Utafiti na Habari cha Knesset kuhusu wimbi lisilo na mfano wake la watu kukimbia Israel zinaonyesha kuwa mgogoro wa utawala huo haujajikita katika ngazi ya kisiasa pekee bali pia katika matabaka ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya kituo hicho, kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, zaidi ya Waisraeli 145,000 walihama na kukimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Idadi hiyo sio tu inazidi ile ya wanaorejea, bali kwa mtazamo wa wachambuzi wa ndani, ni kengele ya hatari kwa mustakabali wa idadi ya watu na kijamii wa Israel. Mnamo Agosti 2024 pekee, karibu watu 50,000 walikimbia kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Kinyume chake, idadi ya waliorejea ilipungua pakubwa katika muda huo, ikionyesha kwamba Israel inapoteza sehemu kubwa ya nguvu kazi yake yenye ujuzi.

Wimbi hili la kukimbia, ambalo Gilad Kario, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamiaji ya Knesset amelitaja kama “tsunami ya idadi ya watu,” ni ishara ya kuporomoka imani ya umma kuhusu mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa Israel. Watu ambao huko nyuma walitamani kurudi katika eti “nchi ya ahadi” sasa wanakimbia na kuiacha kwa hofu kubwa. Kario amesisitiza kwa usahihi kwamba, uhamaji huu usioepukika, ni matokeo ya moja kwa moja ya siasa za baraza la mawaziri la sasa, ambalo limegawanya jamii katika sehemu mbili na kulemaza mfumo wa kijamii.

Maelfu wa Waisraeli wanatoroka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina

Katika uga wa kisiasa, Israel inasumbuliwa na aina fulani ya mkanganyiko. Katika muda wa chini ya miaka miwili, mawaziri watatu wa mambo ya nje wameteuliwa kwa sababu za kisiasa tu, ambapo usimamizi wa wizara ya mambo ya nje umevurugwa na kuangukia mikononi mwa washauri wa karibu wa waziri mkuu. Mgogoro huu wa kisiasa umeambatana na uzembe wa kitaasisi, kuanzia kusimamishwa kwa muda mrefu uteuzi wa mkuu wa huduma ya ujasusi hadi kujiuzulu kwa maafisa wakuu wa usalama na kushuhudiwa mizozo kati ya taasisi za usalama na jeshi. Kinachoendelea sasa huko Israel ni aina fulani ya kuporomoka kwa utaratibu wa kisiasa ambapo mfumo wa bunge la Israel pia umekuwa uwanja wa mivutano ya makundi, ufisadi wa kiutawala na maamuzi ya kibinafsi.

Katika upande mwingine, katika hali ambayo dunia inatazama upya uhusiano wake na Palestina ambapo zaidi ya nchi 140 zimelitambua rasmi taifa huru la Palestina, Israel inajikuta katika hali isiyo ya kawaida ya kutengwa kidiplomasia. Uhusiano wa Tel Aviv na Ulaya umekuwa baridi, ambapo hata washirika wake wa jadi nchini Marekani wanajitenga taratibu na sera kali na zisizo imara za baraza la mawaziri la Netanyahu. Kwa hakika, serikali ya Netanyahu haijawahi kutengwa kiasi hiki katika jukwaa la kimataifa, na pia imepoteza uhalali wake wa kisiasa nyumbani.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, hali ni mbaya sana. Uamuzi wa Mfuko wa Utajiri wa Kitaifa wa Norway wa kuondoa mitaji yake katika benki na makampuni ya Israel ni mfano mmoja tu wa mwelekeo mpana unaoakisi hali ya utawala huo kutengwa kiuchumi. Moja baada ya lingine, makampuni ya kimataifa yanajiondoa taratibu katika miradi ya Israel. Pengo kati ya tabaka la kati na wasomi wa masuala ya uchumi limeongezeka na bei ya nyumba na gharama ya maisha zimefikia viwango visivyo na mfano wake, suala ambalo limechochea hisia za kukata tamaa na kutokuwa na utulivu kati ya matabaka ya wasomi na vijana.

Wakati huo huo, siasa za kufurutu ada za baraza la mawaziri la mrengo wa kulia la Netanyahu zimewafanya raia wengi wahisi kuwa serikali haiwawakilishi tena. Maandamano makubwa ya miaka ya hivi karibuni dhidi ya mageuzi ya mahakama na sera za baraza la mawaziri la Netanyahu ni kielelezo cha kukasirshwa huku kwa umma. Kwa upande mwingine, kuendelea vita ndani ya Israel kumeongeza hali ya ukosefu wa usalama katika jamii nzima ya utawala huo.

Mgogoro wa sasa wa Israel ni matokeo ya wakati mmoja ya kuporomoka kisiasa, kutengwa kiuchumi na mgawanyiko wa kijamii. Kila moja kati ya mambo haya huchochea jingine. Mgogoro wa kisiasa huchochea kutoaminiana kiuchumi, uchumi dhaifu huzidisha uhamiaji na kukimbia watu, na uhamiaji huharibu mshikamano wa kijamii. Kwa utaratibu huu, mzunguko wa kuporomoka utawala wa Israel umeanza ambapo iwapo hautasimamishwa, utafikia mwisho wake kupitia utawala wa Netanyahu.

Israel

Kwa vyovyote vile, kile kinachosikika leo kutoka kwa Lapid sio ukosoaji wa mwanasiasa wa upinzani tu, bali ni onyo la ukweli wa kihistoria. Israel imefikia hatua ambayo haiwezi tena kuficha migongano yake ya ndani kupitia ukandamizaji au propaganda za kisiasa. Ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, utawala ghasibu wa Israel hatimaye utasambaratika, si kutokana na tishio la nje, bali mmomonyoko wa ndani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *