
Rais wa Kenya, William Ruto, ametetea hatua yake ya kusaini miswada minane kuwa sheria mnamo Oktoba 15, 2025—siku hiyo hiyo ambayo taifa lilipokea taarifa za kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga.
Katika mazishi ya baba wa Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, yaliyofanyika Thome, Kaunti ya Laikipia, Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto, amezungumzia miswada minane aliyosaini kuwa sheria mnamo Oktoba 15, siku ambayo taifa lilipokea taarifa za kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga.
Rais Ruto amesema kuwa alikamilisha majukumu yake ya kikatiba kabla ya kufahamishwa kuhusu msiba huo. Ameeleza kuwa kusaini miswada hiyo ilikuwa sehemu ya ratiba yake rasmi ya siku hiyo, na kwamba miswada hiyo inalenga kulinda watoto na jamii dhidi ya madhara ya kidijitali—ikiwemo Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni.
Akinukuliwa, Rais Ruto amesema: “Tuseme ukweli, kuna watu wanatafuta kuchafua Kenya kwa mbinu zote. Hii sheria ilikuwepo, na mabadiliko yalianza mwaka 2024 kupitia Bunge. Mimi niliamka Jumatano, na hiyo ndiyo ilikuwa kazi yangu siku hiyo. Na ilikuwa kazi ya kikatiba ya kutia sahihi.”
Amesisitiza kuwa hakuna cha kuficha katika sheria hiyo, akiongeza kuwa misimamo mikali ya kidini yenye madhara kama ya tukio la Shakahola lazima yazuiwe. Aidha, amesema vijana wa Kenya wanaangamizwa na maudhui machafu katika mitandao ya kijamii, na serikali lazima ichukue hatua kukomesha ufuska huo. Vilevile, ametoa wito kwa serikali kuzuia matumizi ya mitandao ya kijamii kueneza ugaidi, ili kulinda usalama wa taifa.
Hata hivyo, hatua hiyo imezua mjadala mkali. Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Jaji Mkuu wa zamani, David Maraga, wamekosoa miswada hiyo wakidai kuwa ni ya kiimla na isiyo halali.