
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba hali ya kutoadhibiwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, ambayo imepewa uhalali na wale wanaounga mkono utawala huo, inapaswa kukoma mara moja.
Ismail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, alirejelea hukumu ya ushauri ya tarehe 22 Oktoba 2025 iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini The Hague, ambayo ililaani hatua za utawala wa Kizayuni za kuzuia shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa Misaada Kwa Wapalestina, UNRWA, na kulazimisha njaa na ukosefu wa chakula kwa watu wa Gaza.
Akiashiria maoni hayo ya mahakama, Baqaei alisema: “Maoni ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu Palestina yanathibitisha kwa mara nyingine ukweli usiopingika kwamba utawala wa Israel ndio mvunjaji mkubwa zaidi wa kanuni zote za sheria za kibinadamu za kimataifa.”
Baqaei alihitimisha kwa kusisitiza:
“Hali hii ya kutoadhibiwa ambayo imekuwa ikiendelezwa na wale wanaounga mkono na kutetea uhalifu wa Israel lazima ikome. Dunia haiwezi tena kunyamazia ukwepaji huu wa uwajibikaji.”
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeitaka Israel ijiepushe kutumia sheria zake za upande mmoja maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na kuukosoa utawala huo ghasibu kwa kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo lililoharibiwa na vita la Gaza.
Katika maoni ya ushauri yaliyotolewa Jumatano iliyopita, Mahakama ya ICJ ilisema kuwa Israel ambao ni “utawala ghasibu”, haina mamlaka rasmi ya kuchukua maamuzi ya kisheria katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds kwa kuzingatia miswada ya unyakuzi iliyopasishwa jana na Bunge la Israel (Knesset).
Yuji Iwasawa, Mwanasheria Mashuhuri wa Japan na mkuu wa sasa wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) pia ameukosoa utawala wa Tel Aviv kwa kusitisha ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Iwasawa ameitaka Israel iwezesha programu zote za utoaji misaada kwa Wapalestina wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu akisema kuwa mahakama ya ICJ kwa kauli moja inaamini kuwa Israel ambao ni utawala ghasibu inawajibika kutekeleza majukumu yake ya kisheria.
Mwanasheria huyo Mashuhuri wa Japan pia ametangaza kuwa uamuzi wa pamoja umefikiwa kuhusu marufuku ya kutumiwa njaa kama silaha ya vita, akimaanisha kitendo cha Israel cha kulipiga marufuku kufanya kazi Ukanda wa Gaza shirika la UNRWA ambalo ni mtoaji mkuu wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo.