
Rais wa zamani wa Madagascar, Andry Rajoelina, amevuliwa uraia wake baada ya kuikimbia nchi hiyo mapema mwezi huu kufuatia maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana dhidi ya utawala wake.
Taarifa hii imetolewa huku mshauri wa zamani wa Andry Rajoelina, Maminiaina Ravatomanga akitiwa mbaroni huko Mauritius akishukiwa kutakatisha dola milioni 160 mali ya serikali.
Ravatomanga ambaye alikimbilia Mauritius baada ya Rajoelina kuondoka Madagascar, alikuwa amewekwa chini ya uangalizi wa polisi na maafisa wa Kamisheni ya Jinai za Fedha (FCC) katika zahanati binafsi huko Port Louis ambako alikwenda kwa ajili ya matibabu.
Mshauri huyo wa zamani wa Rais wa Madagascar aliyeondolewa madarakani, alikamatwa akituhumiwa kutakatisha dola milioni 165.
Siddartha Wahaldar, wakili anayemtetea Maminiana Ravaromanga amethibitisha kuwa mteja wake huyo yupo kizuizini. Hata hivyo hakutaja anakabiliwa na tuhuma zipi.
Wiki za mwisho za kuwepo madarakani Andry Rajoelina ziliathiriwa na maandamano ya maelfu ya wananchi wa Madasgascar waliokuwa wakilalamikia tatizo la umeme, ukosefu wa maji, kupanda gharama za maisha na ufisadi.
Serikali mpya ya Madagascar imetangaza kuwa inamvua uraia Rajoelina kwa sababu alipata uraia wa Ufaransa mwaka 2014 kinyume na sheria ya Madagascar.
Kiongozi wa Mapinduzi nchini Madagscar, Michael Randrinanirina, aliapishwa kuiongoza nchi hiyo tarehe 17 mwezi huu na kuahidi kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miaka miwili.