
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Tehran iko tayari kushiriki katika mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani ili kufikia “suluhisho la busara” kuhusu suala la nyuklia, kwa misingi ya usawa na kuheshimiana pande zote.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha mtandaoni yaliyochapishwa Jumamosi, Araghchi alisisitiza kuwa: “Iran imetangaza mara kadhaa kuwa haijawahi kuacha na haitakataa kamwe njia ya diplomasia.” Ameongeza kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo na Marekani “iwapo Wamarekani wako tayari kujadiliana kwa dhati na kwa nia njema ili kufikia makubaliano yenye manufaa kwa pande zote, si ya upande mmoja, na yawe kwa misingi ya usawa na kuheshimiana.”
Araghchi alisisitiza kuwa: “Hatutakubali kuacha haki za watu wa Iran, wala hatutavumilia ukandamizaji na vitisho dhidi yao; hata hivyo, tuko tayari kwa suluhisho lolote la busara.” Alirudia msimamo wa Iran kuwa haina haja ya silaha za nyuklia, akisema kuwa “uwezo wa Iran wa kusema hapana kwa mataifa yenye nguvu” ndio “bomu lake la atomiki,” jambo ambalo limekuwepo tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.
Mwanadiplomasia huyo mkuu amebainisha kuwa “tatizo kati ya Iran na Marekani ni hulka ya ubabe ya upande wa pili.”
Amesema Tehran ilikuwa ikifanya mazungumzo na Marekani kuhusu mpango wake wa nishati ya nyuklia ili kujenga imani na kutoa hakikisho kuwa hakuna mwelekeo wa kijeshi katika mpango huo. .
Araghchi amesema kuwa pande hizo mbili zilikuwa zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja chini ya upatanishi wa Oman na duru ya sita ilikuwa ifanyike Juni 15, lakini “utawala wa Israeli ulianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran siku mbili kabla ya mazungumzo hayo.”
Waziri huyo amesisitiza kuwa mapambano ya Iran katika vita vya siku 12 vya Israel na Marekani dhidi ya nchi hiyo mwezi Juni yalikuwa “tukio la kihistoria.” Aliongeza kuwa: “Dunia nzima inapaswa kuelewa kuwa Wairani hawakai kimya mbele ya dhulma, shinikizo, na vita, bali wanapinga.”
Katika kipindi hicho cha siku 12, alisema, Wairani walithibitisha kuwa hawatawahi kuacha haki zao wala kukimbia vita, bali wamesimama imara na kupinga. Araghchi alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa Iran kuendelea kuwa tayari, lakini akaongeza kuwa “hii haimaanishi kuwa kuna uwezekano wa vita vipya.”