Mapigano yamezidi kushadidi maeneo kadhaa ya Sudan baada ya waasi wa RSF kuendeleza mashambulizi dhidi ya mji wa el-Fasher ulioko Kaskazini mwa Darfur, pamoja na mji wa Bara katika mkoa wa Kordofan Kaskazini.

Waasi wa RSF walishambulia Bara, mji ulio takribani kilomita 350 kusini magharibi mwa mji mkuu Khartoum, kutoka pande kadhaa asubuhi ya Jumamosi.

Kundi hilo la RSF lilichapisha video siku ya Ijumaa likidai kuwa wapiganaji wake wametwaa makazi ya gavana wa Darfur Kaskazini huko el-Fasher, na sasa wako karibu na makao makuu ya Idara ya 6 ya Jeshi la Kitaifa la Sudan (SAF), ambayo ni muhimu katika uongozi wa kijeshi wa eneo hilo.

Katika video hizo, wapiganaji wa RSF walidai kuwa watafika hadi katikati ya mji. Wakati huohuo, jeshi la Sudan limetangaza kuwa limefanikiwa kuzuia shambulio hilo kubwa la RSF katika Al Fasher kutoka pande tano, katika moja ya mapigano makali zaidi ambayo mji huo umeshuhudia katika kipindi cha miezi kadhaa.

Aidha, serikali ya Sudan imeitaka jamii ya kimataifa, pamoja na mashirika ya kikanda na yale ya haki za binadamu, kulaani uhalifu unaofanywa na waasi wa RSF dhidi ya raia na kuchukua hatua za haraka za kuvikomesha. Katika tamko lililotolewa Jumamosi, serikali ilisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti kuwawajibisha wahalifu hao na waungaji mkono wao, ili kulinda raia na kutetea haki za binadamu.

Wakati huohuo, mashirika manne ya Umoja wa Mataifa (UN) yameonya wiki hii kuwa maelfu ya watoto wako hatarini kufa, huku zaidi ya raia 250,000, nusu yao wakiwa watoto , wakiwa hawana huduma za chakula na afya kutokana na mzingiro wa miezi 16 wa el-Fasher.

Jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023, vita ambavyo tayari vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na kupelekea zaidi ya watu milioni 14 kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *