Mkuu wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema: Vita vya Gaza vimeonyesha kwamba sheria za kimataifa hazizingatiwi kabisa.

Philip Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huku akisema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 80 iliyopita haujawahi kupuuza juhudi zozote za kuleta amani, kupambana na umaskini na njaa, kutetea haki za binadamu na kuimarisha ulimwengu unaozingatia sheria, amesisitiza kuwa kufungamana upya na misingi hiyo ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote hasa katika muktadha wa maafa ya Gaza, ambapo tumeshuhudia kutozingatiwa kabisa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya misaada ya kibinadamu kama silaha.

Msimamo wa Lazzarini unaweza kuchukuliwa kuwa jibu kwa juhudi za Israel na baadhi ya washirika wake za kutaka kudhoofisha na kufutilia mbali nafasi ya UNRWA katika kutoa misaada kwa wananchi wa Palestina, juhudi ambazo, kwa kuzingatia madai yasiyo na msingi, zinalenga zaidi ya masuala ya kiusalama na inaonekana ni sehemu ya mkakati mpana wa kutwaa udhibiti kamili wa Gaza na kuondoa huko taasisi huru za kimataifa.

UNRWA ilianza kazi zake mwaka 1949 kama kitengo cha utendaji cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa Kipalestina, na kwa miongo kadhaa iliyopita, imetoa huduma muhimu katika nyanja mbalimbali za elimu, afya, lishe, makazi na misaada ya dharura kwa mamilioni ya Wapalestina wanaoishi Gaza, Ukingo wa Magharibi, Jordan, Lebanon na Syria. Taasisi hii sio tu ni shirika la kutoa misaada ya kibinadamu bali pia ni ishara ya kujitolea kwa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kutetea haki za wakimbizi wa Kipalestina na kuhifadhi utu wao wa kibinadamu dhidi ya siasa za uvamizi, kubaguliwa na kukanyagwa haki zao.

Pamoja na hayo, katika vita vya Gaza, Israel ikiungwa mkono na washirika wake wa Magharibi, imejaribu kuiondoa taasisi hii muhimu kwenye medani na kuvuruga shughuli zake kutokana na sababu mbalimbali za kisiasa na kiusalama, kama tulivyoshuhudia katika miezi ya mwisho ya vita vya Gaza, ambapo UNRWA ilizuiwa kabisa kutoa misaada ya dharura kwa Wapalestina. Madai makuu ya Israel na washirika wake, ambayo yalirudiwa na Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani siku chache zilizopita, ni kwamba UNRWA imekuwa “tawi la Hamas” na kuwa haiwezi kuwa na nafasi katika mustakbali wa Gaza. Hii ni pamoja na ukweli kwamba Umoja wa Mataifa umekanusha mara kwa mara madai hayo na kusisitiza kuwa hakuna ushahidi wowote wa maana uliotolewa kuthibitisha upenyaji wa Hamas katika UNRWA.

Philip Lazzarini

Katika ripoti za hivi karibuni, UNRWA imesema mamia kwa maelfu ya watu huko Gaza wanahitaji msaada wa haraka na kwamba shirika hilo ndilo shirika pekee ambalo lina miundombinu, uzoefu na mtandao wa kibinadamu unaowezesha kutolewa huduma hizi. Hata hivyo, Israel na washirika wake katika vita vya Gaza, licha ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo kwa uwazi inaitaka Israel kuwezesha kuingia misaada ya kibinadamu katika ukanda huo, ikiwa ni pamoja na UNRWA, wamezuia UNRWA kutoa misaada na huduma za dharura huko Gaza, na wanaendelea kukaidi amri hiyo.

Kuhusiana na suala hili, Philip Lazzarini, mkuu wa UNRWA, alisisitiza katika taarifa yake hivi karibuni kwamba matumizi ya misaada ya kibinadamu kama silaha ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kusimama imara dhidi ya ukiukaji huo. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, mara kwa mara wametoa wito wa Israel kuzingatia sheria na kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kufikishwa misaada kwa wananchi wa Palestina, na kusisitiza kuwa kuzuia kuingia kwa misaada na kupiga marufuku shughuli za UNRWA ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Kuhusiana na hilo, inaonekana kuwa, jaribio la Israel la kuiondoa UNRWA uwanjani ni sehemu ya mkakati mkubwa zaidi wa kuchukua udhibiti kamili wa Gaza na kuliondoa shirika lolote huru la kimataifa linaloweza kuakisi sauti ya wananchi wa Palestina duniani.

Huku maafa ya kibinadamu huko Gaza yakifikia hatua hatari ya mgogoro, ni wazi kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuunga mkono UNRWA kwa nguvu zake zote, kuweka wazi njia ya misaada na kutoruhusu visingizio vya kisiasa kutishia maisha ya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia. Kwa hakika, kuwekwa vizuizi au kudhoofishwa UNRWA kunatuma ujumbe hatari kwa ulimwengu: Kwamba haki za binadamu na sheria za kibinadamu zinaweza kukiukwa wakati wowote kwa visingizio visivyo na msingi. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kwamba sehemu ya mustakbali wa Palestina, hususan huko Gaza, inafungamana moja kwa moja na uwezo na uhuru wa UNRWA, ambapo uzembe wowote katika uwanja huu utaisababishia jamii ya mwanadamu madhara makubwa yasiyofidika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *