Bi. Catherine Connolly, mgombea wa mrengo wa kushoto katika uchaguzi wa urais nchini Ireland ambaye anajulikana kwa misimamo yake ya kuunga mkono Palestina, ameibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya kura, yaliyomuonyesha Connolly akiwa mbele kwa tofauti kubwa, Heather Humphreys, mgombea wa chama cha mrengo wa kulia Fine Gael, alikubali kushindwa jioni ya Jumamosi.

Matokeo ya kuhesabu takribani theluthi mbili ya kura za uchaguzi huo yanaonyesha kuwa Connolly amepata asilimia 64 ya kura, na hivyo kuwa mshindi wa wazi wa kiti cha urais wa Ireland.

Connolly, mwenye umri wa miaka 68, amefanikiwa kushinda kwa kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wa Ireland. Katika masuala ya sera za nje, amekuwa mwanasiasa mwenye msimamo thabiti wa kuunga mkono Palestina, huku akionyesha ukosoaji mkali dhidi ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Akizungumza mwezi uliopita katika kipindi cha Morning Ireland cha kituo cha redio RTÉ, Catherine Connolly alisema kuwa Israel inajihusisha na vitendo vinavyofanana na vya dola la kigaidi. Aliendelea kusema Harakati ya Hamas ilichaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa mwisho na ilipata uungwaji mkono mkubwa na hivyo ni sehemu ya jamii ya kiraia ya Palestina.

Bi Connolly, ambaye amekuwa akihudhuria maandamano ya kuunga mkono Palestina nchini Ireland, pia alimkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, baada ya kutangaza kuwa Hamas haitakuwa na nafasi yoyote katika serikali mpya, wakati huo huo akitambua rasmi taifa la Palestina.

Alisema: “Ninatoka Ireland, nchi ambayo ina historia ya kukoloniwa. Ningekuwa mwangalifu sana kujaribu kuwaelekeza watu wa taifa huru namna ya kuendesha nchi yao.”

Alisema Wapalestina wenyewe wanapaswa kuamua, kwa njia ya kidemokrasia, ni nani wanayetaka awaongoze.

Katika chapisho aliloweka kwenye Instagram wiki hii, Connolly aliongeza: “Israel imefanya mauaji ya kimbari huko Gaza. Kuona au kuufanya mauaji ya kimbari kuwa jambo la kawaida ni janga kubwa kwa watu wa Palestina — na ni janga kwa ubinadamu wote.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *