Rais Vladimir Putin wa Russia amezindua kombora jipya linalotumia fueli na mafuta ya nyuklia linaloitwa Burevestnik wakati wa kukagua kituo cha mstari wa mbele cha vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, wakati wa ziara yake katika kituo cha mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine, Rais wa Russia amezindua kombora hilo la Burevestnik, ambalo “halina mfano wowote duniani” na linaweza kutumika “dhidi ya maeneo yenye ulinzi mkali popote pale duniani.”

Kombora hilo, ambalo lilifanyiwa jaribio lake la mwisho mwaka wa 2023, linaendeshwa na mtambo wa nyuklia na lina uwezo wa kubeba kichwa cha silaha za atomiki.

Akizungumzia kuzingirwa zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Ukraine katika maeneo ya Kharkiv na Donetsk, Rais Putin ametaka hatua zichukuliwe ili kupunguza idadi ya majeruhi kati ya wanajeshi wa Ukraine wanaokusudia kujisalimisha.

Amebainisha kuwa, “Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine waliojaribu kujisalimisha wanapigwa risasi mgongoni (na vikosi vyao wenyewe).”

Rais Putin pia amesema kwamba jeshi la Ukraine linatumia raia kama ngao za binadamu, lakini “hatua zote muhimu zitaendelea kuchukuliwa daima ili kuhakikisha raia wanaotumiwa kama ngao na wanajeshi wa Ukraine wanalindiwa usalama wao.”

Mara baada ya Rais Putin kuwasili kwenye eneo hilo la mstari wa mbele wa vita huko Ukraine, Kamanda wa Jeshi la Russia Valery Gerasimov ametangaza habari ya kuzingirwa zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Ukraine katika maeneo mawili tofauti. Amesema kwamba wanajeshi 5,000 wa Ukraine wamezingirwa na wanajeshi wa Russia huko Kopiansk, mkoa wa Kharkiv na 5,500 wengine wamezingirwa huko Krasnoarmeysk, mkoa wa Donetsk.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *