Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kusikitishwa kwake na chapisho la shirika la Amnesty International lenye kichwa cha habari ‘Wimbi la Ugaidi’ Laikumba Tanzania Kabla ya Kura ya 2025″.

Taarifa ya serikali ya Tanzania imesema, ingawa Tanzania iko wazi kwa ushirikiano wa kujenga na washirika wa kimataifa, lakini inasikitisha kwamba Amnesty International imechagua kuchapisha madai makubwa na yasiyo na uthibitisho bila kuipa Serikali fursa nzuri ya kujibu kabla ya kutolewa kwake.

Hatua hiyo inadhoofisha kanuni za usawa na heshima ya pande zote ambazo zinapaswa kuongoza mazungumzo ya kimataifa ya haki za binadamu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Tanzania inathibitisha tena dhamira yake thabiti ya kulinda na kukuza haki za binadamu, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (pamoja na marekebisho yake), na kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na ya kikanda ya haki za binadamu ambayo Tanzania ni mwanachama, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, na Mkataba wa Kupinga Mateso.

”Uwasilishaji wa taarifa hiyo kuhusu Tanzania kama nchi inayoruhusu kukamatwa kiholela, kutoweka kwa watu kwa kulazimishwa, na kukandamiza uhuru wa raia hauendani na mifumo ya kisheria na taasisi zilizopo. Tanzania inatekeleza sera ya kutovumilia kabisa mateso na aina nyingine za adhabu au matendo ya kikatili na ya kinyama”.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumatano ya wiki hii 29 Oktoba, Watanzania waliotimiza masharti ya kupiga kura wanatarajiwa kuuelekea katika vituo vya kuupigia kura kwa ajili ya kumchaguua Rais, Wabunge na madiwani.

Wapinzani nchini Tanzania wamekuwa wakidai kukandamizwa huku baadhi ya wagombea wao wakizuiwa kugombea nafasi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *