
Asasi isiyo ya kiserikali ya Morocco imesema kwamba zaidi ya watu 1,500 walioshiriki katika maandamano yaliyoenea katika kona zote za Morocco wakidai huduma bora ya afya, elimu na kukomeshwa ufisadi, wamefunguliwa mashtaka na serikali. Maandamano hayo yalidumu kwa mwezi mzima.
Kwa mwezi mmoja sasa vijana wa Morocco wamekuwa wakiandamana mitaani kama sehemu ya harakati ya Gen Z 212 kupinga kupanda gharama za elimu, huduma ya afya na serikali ya kidikteta nchini humo.
Chama cha Morocco cha kutetea haki za binadamu (ADMH) ambacho ni NGO ya eneo hilo, kimesema kabla ya mwishoni mwa wiki kwamba maandamano hayo yamesababisha kufunguliwa mashtaka 1,500 ya watu walioshiriki katika maandamano hayo. Inakadiriwa kuwa, watu 1000 wanashikiliwa korokoroni hivi sasa.
Baadhi ya waandamanaji tayari wameshafunguliwa mashtaka. Mahakama ya Agadir imeendesha kesi za watu 240 na kuwahukumu watu 39 kifungo cha miaka 6 hadi 15 jela.
Katika siku za hivi karibuni, maandamano yamepungua sana huko Morocco kutokana na harakati hizo kupoteza nguvu na mvuto.
Mfalme Mohammed VI wa Morocco, alitangaza tarehe 10 Oktoba 10 kwamba mageuzi ya kijamii yangeharakishwa na serikali iliahidi kufanya juhudi ambazo hazijawahi kutokea kwa gharama ya euro bilioni 13 kwenye bajeti ya 2026 ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na elimu.
Chama cha Morocco cha kutetea haki za binadamu (ADMH) kimetoa mwito wa kuachiliwa huru wote waliotiwa mbaroni na imetaka pia kesi zao ziendeshwe kwa haki.