
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kwa robo mbili mfululizo, Airtel Tanzania imefanikiwa kupunguza matukio ya jaribio la udanganyifu kwa asilimia 12.5, ikilinganishwa na watoa huduma wengine wa mawasiliano.
Mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mfumo wa Akili Unde (AI) wa kugundua spam na kutoa tahadhari za udanganyifu.
Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, inaonesha kuwa Airtel Tanzania imepunguza matukio ya jaribio la udanganyifu kutoka 2,595 yaliyorekodiwa Juni hadi 1,559, sawa na punguzo la 1,036.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonesha kuwa kwa jumla, majaribio ya udanganyifu kwa kampuni zote tano yamepungua kwa asilimia 10, kutoka 13,837 hadi 12,475, huku mikoa ya Rukwa na Morogoro ikiongoza kwa idadi kubwa ya matukio ya majaribio ya udanganyifu.
Ripoti hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari, inaonesha kuwa mikoa ya Rukwa na Morogoro imerekodi idadi kubwa ya majaribio ya udanganyifu, ikifuatiwa na Dar es Salaam, Mbeya na Kilimanjaro ambazo zimeshika nafasi ya tatu, nne na tano mtawalia.
Ripoti hiyo inaonesha pia kuwa mikoa ya Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba imerekodi idadi ya chini zaidi ya majaribio ya udanganyifu.
“Kwa ujumla, utendaji wa robo hii unathibitisha kasi kubwa kuelekea Tanzania iliyounganishwa, salama, jumuishi na yenye nguvu za kidijitali. TCRA inabaki imejitolea kuwezesha mazingira yanayohimiza uwekezaji kwenye miundombinu, uvumbuzi na ukuaji endelevu wa mfumo wa mawasiliano kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa na dira ya uchumi wa kidijitali,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Mwaka huu, Airtel Tanzania imezindua Spam Alert – Kataa Matapeli, mfumo wa kwanza barani Afrika wa Akili Unde (AI) unaogundua spam na kutoa tahadhari za udanganyifu.
Huduma hiyo inatumia AI kubaini ujumbe unaoshukiwa na kutoa tahadhari kwa watumiaji kwa wakati halisi ili kuwasaidia kuepuka udanganyifu.
Kifaa hicho cha ubunifu kilizinduliwa kama sehemu ya kampeni ya kitaifa ya #SITAPELIKI ya kupambana na udanganyifu na kuunganisha Airtel Tanzania na juhudi za Serikali za kuongeza usalama wa watumiaji wa simu, kilichozinduliwa Februari mwaka huu.
Ripoti ya TCRA inaonesha kuwa Vodacom inaongoza kukumbwa na majaribio ya udanganyifu kwa asilimia 31.9, ikifuatiwa na Yas kwa asilimia 19.7, Halotel asilimia 18.2 na TTCL asilimia 17.8.
Akizungumzia kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masuala ya Udhibiti wa Airtel, Beatrice Singano, amesema: “Matokeo ya kampeni ya Airtel Kataa Matapeli yanaonekana wazi. Majaribio ya udanganyifu yamepungua kutoka asilimia 19 hadi 12 kufikia Septemba. Punguzo hili la pointi saba linaonyesha ufanisi wa tahadhari za spam zinazochukua hatua mapema.”
Singano amesema huduma ya Airtel Spam Alert, elimu kwa wateja na hatua madhubuti za usalama zimeleta mabadiliko makubwa katika kukabiliana na majaribio ya udanganyifu.
Ameongeza kuwa wataendelea kuwalinda wateja wao na kuhakikisha mazingira salama ya kidijitali yanaendelea kuwepo muda wote.