MENEJA wa Simba, Dimitar Pantev, amechekelea timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini akawageukia mastaa wa kikosi hicho kuhusu mpango wa kutengeneza mabao mengi.

Pantev hafurahishwi na namna kikosi hicho kinavyotengeneza nafasi na hata kuzitumia kwenye mechi zao na sasa ameanza kupiga hesabu upya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pantev amesema eneo la kwanza ambalo linakwenda kufanyiwa kazi ni lile la kiungo ambalo bado halizalishi mashambulizi mengi.

Kwenye mechi dhidi ya Nsingizini Hotspurs juzi Jumapili, Simba ilitengeneza nafasi kubwa tatu tu za wazi za kuzalisha mabao, jambo ambalo limemkera kocha huyo baada ya kushindwa kuzitumia na kufanya matokeo kuwa 0-0, lakini imefuzu makundi baada ya ugenini kushinda 3-0.

SIMB 01

“Bado hatuna ubunifu mkubwa pale katikati ya uwanja, viungo wetu lazima tuongeze namna ya kutengeneza nafasi nyingi zaidi, kila kiungo sasa namjua uwezo wake, wachache sana sijawaona,” amesema Pantev.

“Ukichezea timu kubwa kama Simba lazima uonyeshe ukomavu, kila wakati watu wanatarajia makubwa kutoka kwako, sasa tutakwenda kuwaongezea ubora.”

SIMB 02

Aidha, Pantev aliongeza kuwa licha ya changamoto hiyo ya eneo la kiungo, pia kocha huyo raia wa Bulgaria ameshtuka juu ya changamoto ya washambuliaji wake kwenye kutumia nafasi.

“Sio tu viungo, hata kule mbele washambuliaji wetu bado tunatakiwa kuwaongezea kitu, hatupeleki presha kubwa kwenye eneo la mwisho.

“Kuna wakati tunakuwa sawa, lakini kuna wakati tunarudi tena chini, tunahitaji kuwa na mwendelezo wa kutumia nafasi, haya yote tutakwenda kuyafanyia kazi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *