
Nyota wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher amesema anaamini kuna matatizo ndani ya timu hiyo yanayopelekea ifanye vibaya katika Ligi Kuu England (EPL) msimu huu na yanatakiwa kutatuliwa.
Carragher alishuhudia timu hiyo ikipokea kichapo cha mabao 3-2 Jumamosi iliyopita kutoka kwa Brentford kilichoifanya ianguke hadi katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Kana kwamba haitoshi, hicho kilikuwa kipigo cha nne mfululizo kwa Liverpool kwenye EPL msimu huu, matokeo ambayo yameonekana kutowafurahisha mashabiki wengi wa timu hiyo.
Miongoni mwao ni Carragher ambaye hadhani kwamba ni jambo la kawaida kwa timu kama Liverpool kupoteza mechi nne mfululizo tena kati ya tisa za mwanzo hivyo anaamini timu hiyo inapitia katika matatizo.
“Sidhani kama wana fiziki ya kutosha. Kupoteza mechi nne mfululizo kwa timu kama Brentford au nyingine inayopambana kutoshuka daraja ingekuwa ni majanga.
“Kuona mabingwa wanapoteza mechi nne mfululizo tena kwa matumizi yaliyofanyika wakati wa kiangazi, nadhani tupo katika matatizo.
“Kutakuwa na maswali mengi yataulizwa kwa kila mmoja, wachezaji na meneja,” amesema Carragher.
Kuruhusu mabao matatu kwenye mchezo huo, kumeifanya Liverpool iwe imefungwa mabao tisa katika mechi nne zilizopita za Ligi Kuu England.