Afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza dhamira isiyoyumba ya harakati hiyo ya kutekeleza usitishaji vita huko Gaza na kusema Wapalestina hawataki kitu chochote isipokuwa haki yao inayotambulika kimataifa ya kuwa na nchi huru.

Khalil al Hayya, kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza ameeleza kuwa upande wa Palestina una azma kubwa na ya kutosha ili kuhakikisha kuwa vita havijiri tena na kwamba Hamas haiupatii kisingizio chochote utawala wa Kizayuni cha kuanzisha tena vita. 

Amesema, jamii ya kimataifa pia haitaruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel kurejea vitani. 

“Hamas iko jadi kuhusu mapatano yaliyofikiwa na inatoa kipaumbele kwa suala la kukabidhi haraka mateka. 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amesema kuwa harakati hiyo hadi sasa imeukabidhi utawala wa Israel miili 17 ya mateka wake walioaga dunia na inafanya juhudi za kupata miili mingine 13 iliyosalia.

Khalil al Hayya amesema Hamas haitaacha hata mwili mmoja wa mateka wa utawala wa Kizayuni na kwamba Israel pia haipasi kutumia kisingizio hicho kuendelea kuwadhuru watu wa Palestina. 

Khalil al Hayya pia amezungumzia kufeli Israel huko Gaza na kusema utawala wa Kizayuni umefeli pakubwa kutimiza malengo yake ya kijeshi katika miaka miwili ya vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza. 

Amesema kuwa asilimia kumi ya wakazi wa Gaza wameuawa shahidi, kujeruhiwa au kufungwa jela na wengine hawajulikani walipo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *