Leo ni Jumatatu tarehe 5 Jamadil Awwal mwaka 1447 Hijria sawa na Oktoba 27 mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (sa) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as).

Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo.

Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (as). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (as) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad, mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.   

Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama ‘Siku ya Wauguzi’.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kulijiri vita vya Mu’utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake.

Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Uislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo.

Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, vita hivyo vilijiri kufuatia kuuawa shahidi wakufunzi 14 wa Qur’ani Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Kufuatia mauaji hayo, Mtume aliandaa jeshi la wapiganaji 3000 kwenda eneo hilo lililokuwa chini ya utawala wa Roma. Katika vita hivyo Mtume alimteua Ja’far bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaha kwa kukaimu nafasi hiyo.

Jeshi la Waislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu’utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, na alitoa amri ya kuwataka Waislamu warudi nyuma.

Japokuwa jeshi la Waislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu na mikakati ya jeshi la adui, hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo katika vita vya baadaye.    ****

Siku kama ya leo miaka 465 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la ‘Abus-Suud’, faqihi na mfasiri wa Qur’ani Tukufu.

Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu na aliweza hata kutunga mashairi kwa lugha hizo.

Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na ‘Tafsir Abis-Suud’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafruudhaat.’   

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru.

Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi.

Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.   

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake.

Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.   

Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo.

Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru, ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu. 

Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuondoka madarakani. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo.

Hata kama baada ya miaka 7 Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwaka 1965, lakini alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa.

Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa Jenerali Yahya Khan  aliyekuwa mkwewe. 

Muhammad Ayub Khan

Na siku kama ya leo miaka 52 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani, alimu mkubwa na mtaalamu wa elimu ya fiqhi.

Ayatullah Zanjani alizaliwa mwaka 1308 Hijiria, huku akisomea elimu ya awali na ya juu mjini Zanjan. Baada ya hapo alielekea mjini Qum kwa ajili ya kuendelea na elimu ambapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Abdul-Karim Haeri Yazdi na Muhammad Hujjat Kuh-Kamari. Baada ya Ayatullah Muhammad Hujjat kufariki dunia, Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani alichukua wadhifa wa kuswalisha swala ya jamaa katika shule ya Fayzia.

Aidha katika muongo wa 1320 Hijiria Shamsia, msomi huyo alikutana na Imam Khomeini (MA) ambapo alishirikiana naye katika vikao vingi vya kielimu. Vitabu kama vime ‘Arbain’ ‘Afwahur-Rijal’ ‘Furuqul-Ahkaam’ na vitabu 20 vingine ni sehemu ya turathi za Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani.

Sayyid Ahmad Zanjani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *