Timu 14 zimejihakikishia tiketi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine 16 zimetinga hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mechi za marudiano za raundi ya pili ya mashindano hayo zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyomalizika jana katija miji tofauti Afrika.
Idadi ya timu 16 zitakazocheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakamilika mwishoni mwa wiki hii baada ya mechi mbili zitakazokutanisha timu za RS Berkane dhidi ya Al Ahly Tripoli na mwingine baina ya Pyramids FC.
Tanzania imepata fursa ya kuingiza klabu zote nne kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo ambapo mbili zipo katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni Yanga na Simba huku kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika kukiwa na Azam na Singida Black Stars.
Wawakilishi hao wanne wa Tanzania hata hivyo wanapaswa kujiandaa vilivyo na hatua ya makundi ya mashindano hayo kutokana na uwepo wa timu nyingi zenye uzoefu na nyingine zinazoonekana kuwa na viwango bora kwa siku za hivi karibuni.
Ligi ya Mabingwa Afrika
Kati ya timu 14 ambazo zimeshafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, saba (7) zimewahi kutwaa ubingwa ama wa mashindano hayo au wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa nyakati tofauti.
Timu hizo ni Al Ahly, Mamelodi Sundowns, MC Alger, Stade Malien, JS Kabylie, Esperance na AS FAR.
Orodha hiyo inaweza kuongezeka kufikia tisa iwapo RS Bekane na Pyramids FC zitafanikiwa kuingia hatua ya makundi.
Ukiondoa ubingwa, zipo pia ambazo zimewahi kutinga fainali ama nusu fainali ambazo ni Yanga, Simba na Al Hilal.
Kombe la Shirikisho Afrika
Timu 16 zitakazoshiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika tayari zimeshatimia.
Klabu hizo 16 ni Zamalek, Al Masry, Stellenbosch, Wydad, Olympic Safi, USM Alger, CR Belouizdad, Djoliba, Kaizer Chiefs, Maniema, AS Otoho, FC San Pedro, Nairobi United, Azam FC, Singida Black na Zesco United.
Kati ya timu hizo 16, klabu tatu zimeshawahi kutwaa mataji ya Afrika kwa nyakati tofauti ambazo ni USM Alger, Zamalek na Wydad.