Mali imefunga shule nchini kote kwa muda wa wiki mbili kutokana na uhaba wa mafuta unaoendelea.

Amadou Sy Savane Wazri wa Elimu wa Mali amesema kuwa taasisi za elimu nchini humo zitasimamisha ufundishaji kuanzia leo Jumatatu Oktoba 27 hadi Novemba 9 kufuatia tatizo la mafuta. 

Waziri wa Elimu wa Mali amesema kuwa shule zinatazamiwa kufunguliwa tena tarehe 10 mwezi ujao. 

Kwa wiki kadhaa sasa Mali imekumbwa na mgogoro wa mafuta uliosababishwa na makundi ya wabeba silaha wanaozuia njia na kuweka vizuizi kwenye barabara zinazotumiwa na malori ya mafuta. Hali hii imeathiri pakubwa Bamako mji mkuu wa nchi hiyo. 

Mali, pamoja na nchi jirani za Burkina Faso na Niger, zimekuwa zikikabiliana na hujuma za wanamgambo wenye silaha, ikiwa ni pamoja na makundi yenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na kundi la ISIS yaani Daesh pamoja na waasi wa ndani.

Misururu mirefu imeshuhudiwa kwenye vituo vya mafuta huku usafiri wa umma na teksi za pikipiki zikiwa zimetatizika sana, na kuacha mitaa ya Bamako yenye watu wengi kuwa tulivu isivyo kawaida.

Taasisi za elimu ya juu katika mji mkuu, Bamako pia zimeeleza kuwa zimelazimika kusitisha masomo kwa sababu wanafunzi na walimu wanashindwa kuhudhuria masomo kufuatia uhaba wa mafuta. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *